1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump alitaka kuishambulia Iran wiki chache kabla kuondoka

Mohammed Khelef
17 Novemba 2020

Imefahamika kwamba Rais Donald Trump wa Marekani alikaribia sana kuchukuwa maamuzi ya kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran miezi miwili tu kabla ya kuondoka madarakani, huku Saudi Arabia ikitaka silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/3lO2w
Donald Trump
Picha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Taarifa ya uchunguzi iliyochapishwa jana (Jumatatu, 16 Novemba) na gazeti la New York Times inasema kwamba Trump aliwauliza wasaidizi wake wakuu juu ya uwezekano wa kuvishambulia vinu vya nyuklia vya Iran siku ya Alkhamis iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, kwenye mkutano wake na Makamu wa Rais Mike Pence, Waziri wa Mambo ya Kigeni Mike Pompeo na Mkuu wa Majeshi Jenerali Mark Milley, Trump alitaka kujuwa endapo kuna njia yoyote anayoweza kutumia kuchukuwa hatua dhidi ya maeneo yanayoaminika kuwa na vinu vya nyuklia nchini Iran ndani ya wiki chache kutoka sasa.

Hata hivyo, gazeti la  New York Times linasema kwamba wasaidizi hao wa Trump walimshauri kutokuchukuwa hatua ya kijeshi, wakimuonya kuwa "mashambulizi kama hayo yanaweza kugeuka kuwa mzozo mkubwa" kwenye wiki hizi za mwisho za urais wake.

Sababu ya Trump kuulizia uwezekano huo wa kuishambulia Iran inatajwa kuwa ni ripoti ya Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani (IAEA) iliyosema kwamba Iran inaendelea na kukusanya madini ya uranium yanayotumika kutengenezea silaha za nyuklia.

Uchunguzi wa New York Times umebainisha kwamba maeneo ambayo yangeliweza kushambuliwa na Marekani ni pamoja na Natanz, ambako IAEA inasema kuwa kiwango cha madini ya uranium cha Iran sasa kimeongezeka mara 12 zaidi ya kile kinachoruhusiwa na mkataba wa nyuklia ambao Trump alijiondowa mwaka 2018.

Saudi Arabia yataka silaha za nyuklia

Saudi-Arabien Außenminister Adel al-Dschubeir
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir.Picha: Getty Images/AFP/F. Nureldine

Mkataba huo ambao ulipiganiwa sana na mtangulizi wake, Barack Obama, uliyahusisha pia mataifa mengine matano yenye nguvu duniani, lakini Trump aliiondowa Marekani akidai kuwa ulikuwa unaipendelea sana Iran. 

Taarifa hiyo imeibuliwa wakati Saudi Arabia ikitangaza kwamba nayo ina haki ya kuwa na silaha za nyuklia ikiwa Iran haiwezi kuzuiwa kuwa na silaha hizo.

Kauli hiyo iliyonukuliwa na shirika la habari la Ujerumani, dpa, imetolewa na Waziri wa Mambo ya Mambo ya Kigeni ya Saudi Arabia, Adel al-Jubeir, ambaye alisema: "Hilo ndilo chaguo lililopo. Na Saudi Arabia inaweka wazi kabisa, kwamba itafanya kila iwezalo kuwalinda watu wake na mamlaka yake." 

Mataifa hayo mawili yamekuwa yakiwania udhibiti wa Mashariki ya Kati na Ghuba kwa muda mrefu sasa, huku Saudia ikiungwa mkono na Marekani na ikishirikiana kwa karibu na Israel, kwa mujibu wa taarifa za kijasusi.