1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump abadili msimamo kuhusu makaazi ya Israel

John Juma
3 Februari 2017

Ikulu ya Marekani imesema ujenzi mpya wa makaazi au upanuzi wa makaazi yaliyopo kwa sasa hautasaidia bali utakuwa kizingiti dhidi ya kupatikana kwa amani ya Mashariki ya Kati.

https://p.dw.com/p/2Wu9V
Treffen mit dem US-Präsidenten - May bei Trump
Picha: Reuters/K. Lamarque

Ikulu ya Marekani White House, imeonya kuwa ujenzi zaidi wa makaazi ya Israel katika eneo la Wapalestina huenda usiwe wa manufaa katika kupata suluhisho la amani ya Mashariki ya kati.

"Japo hatuamini kuwa makaazi ya walowezi yaliyopo kwa sasa, ni kizingiti dhidi ya kupatikana kwa amani, ujenzi zaidi wa makaazi mapya au upanuzi wa makaazi yaliyopo kupita mipaka yao kwa sasa, hautakuwa wa usaidizi wowote” Amesema Sean Spicer ambaye ni msemaji wa Ikulu ya White House.

Kauli hiyo ni tofauti na msimamo wa awali ulioshikiliwa na Rais Donald Trump, ambaye alitetea ujenzi wa makaazi hayo ya walowezi unaofanywa na Israel.

Israel yazindua mipango ya makaazi mapya

Makaazi ya walowezi karibu na ukingo wa Magharibi
Makaazi ya walowezi karibu na ukingo wa MagharibiPicha: Getty Images/AFP/T. Coex

Tangu utawala wa Trump ushike usukani, Israel imeidhinisha ujenzi wa makaazi mapya, hatua ambayo wakosoaji wanasema inafanya juhudi za kupatikana kwa suluhisho kati ya Israel na Wapalestina kuwa ngumu.

Katika siku za hivi karibuni Israel imezindua mpango wa kujenga makaazi 3,000 mapya ya walowezi katika Ukingo wa Magharibi. Tangazo kama hilo likiwa la nne katika muda wa chini ya wiki mbili tangu Urais wa Trump uanze..

Spicer amesema, utawala wa Trump haujachukua msimamo rasmi kuhusu makaazi hayo, bali unanuia kuruhusu mazungumzo yaendelee, yakiwemo na waziri wa Israel Benjamin Netanyahu anayetarajiwa kuzuru Marekani na kukutana na Rais Trump tarehe 15 mwezi Februari.

Makaazi katika ukingo wa Magharibi na mashariki ya Jerusalem, yanatizamwa kuwa yasiyokubalika chini ya sheria ya kimataifa na ni kizingiti kikuu dhidi ya amani, kwani yamejengwa katika ardhi ya Wapalestina.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Getty Images/AFP/J. Guez

Uhusiano wa Trump na Netanyahu

Japo rais wa zamani Barrack Obama hakutumia kura ya turufu kupinga uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa uliopinga ujenzi wa makaazi hayo, Rais Trump alitaka Marekani kuupinga uamuzi huo.

Trump amekuwa katika mstari wa mbele kukuza uhusiano mwema na Waziri Mkuu wa Israel Netanyahu, huku akielezea matumaini ya mara kwa mara ya kupatikana kwa suluhisho la amani ya Mashariki ya Kati kwa ujumla.

Trump pia alisema  kabla ya kuingia madarakani kwamba anapanga kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem, hatua ambayo Wapalestina wameipinga vikali.

Kwa muda mrefu, mzozo wa Israel na Wapalestina umekuwa changamoto katika  juhudi za kupatikana kwa amani kati ya pande hizo mbili na eneo la Mashariki ya kati kwa jumla.

Mwandishi: John Juma/APE/AFPE

Mhariri: Yusuf,Saumu