Transparency International yaionya Kenya kutafuta suluhu ya ufisadi | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.03.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Transparency International yaionya Kenya kutafuta suluhu ya ufisadi

Tathmini ya Shirika la kupambana na ufisadi Transparency International tawi la Kenya imebaini kuwa thuluthi mbili ya raia wa Kenya wanaamini kuwa uchaguzi mkuu ujao huenda ukagubikwa na ghasia

Nembo ya Transparency International

Nembo ya Transparency International


Punde baada ya uchaguzi mkuu wa mwezi Disemba mwaka 2007 ghasia zilizuka na yapata watu alfu moja waliuawa na wengine laki tatu kuachwa bila makazi.Nchi za Ghana,Mauritius na Botswana zinasifiwa kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.


Kwa mujibu wa utafiti huo asilimia 64 ya raia wa Kenya wanahofu kwamba ghasia huenda zikazuka tena katika uchaguzi endapo tatizo la ufisadi halitatafutiwa ufumbuzi.

Asilimia 48 kati ya idadi hiyo wanadhani kuwa endapo ghasia hizo zitatokea zitakuwa na athari kubwa zaidi.Uchaguzi mkuu umepangwa kufanyika mwaka 2012.

Tathmini hiyo ya hivi karibuni imeangazia jinsi serikali ya muungano ya Kenya inavyoendesha shughuli zake huku ikigubikwa na madai ya ufisadi.Serikali ya umoja wa kitaifa iliundwa mwaka mmoja uliopita chini ya upatanishi wa Dr Koffi Annan.Hata hivyo serikali hiyo inaripotiwa kusuasua katika masuala ya kufanya mabadiliko ya kisiasa kadhalika ufisadi.

Kulingana na wadadisi ufisadi na rushwa ndio vyanzo vikuu vya purukushani za kisiasa wakati wa uchaguzi.

Orodha ya tathmini ya tatizo la ufisadi ya Shirika hilo imeiweka nchi ya Kenya katika nafasi ya 147 kati ya mataifa 190.

Kulingana na mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Transparency International Job Ogonda nchi ya Kenya inafananishwa na mataifa yanayozongwa na matatizo ya uongozi kama vile Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo au yale yanayojijenga upya baada ya vita kwa mfano Liberia.


Tathmini iliofanywa katika robo ya kwanza ya mwaka huu imebaini kuwa asilimia 76 ya raia wa Kenya wanadhani kwamba serikali haina nia ya kutafuta suluhu ya tatizo la ufisadi.Utafiti huo ulifanyiwa watu alfu moja kutoka sehemu zote za nchi.

Ikifafanua zaidi asilimia 25.6 ya raia wa Kenya wanalilaumu bunge,asilimia 24.5 wanaunyoshea kidole mfumo wa mahakama na asilimia 17.9 iliyosalia inalaumu serikali kuu.

Kwa upande mwengine asilimia 51 ya raia wa Kenya wanatoa wito wa sheria kuwatia hatiani watu wengi zaidi wanaotuhumiwa kwa ufisadi,asilimia 32 wangependa uchaguzi mpya ufanyike kabla ya mwaka 2012 na asilimia 69 walieleza kuwa endapo uchaguzi utafanyika hivi sasa na wabunge waliopo watawania tena nyadhifa hizo huenda wasiwachague.

Mwenyekiti wa Shirika la linalohusika na uangalizi wa masuala ya ufisadi Transparency International Bibi Huguette Labelle ameeleza kuwa maendeleo ya aina yoyote ile yanategemea amani na taasisi zinazozingatia masuala ya uaminifu likiwemo lile la haki na uwazi. Amesisitiza kuwa athari kubwa zinaripotiwa katika sekta ya siasa. ''Vyama vya kisiasa vimekuwa vikiongoza katika orodha ya taasisi za serikali zinazoathiriwa na ufisadi kama wanavyodhani raia wa nchi husika.Taasisi zinazofuatia ni wabunge,maafisa wa polisi,mahakama na sekta binafsi zote hizo ziko katika nafasi tano za mwanzo za orodha hiyo.''


Serikali kwa upande wake imekiri kuwa ufisadi umekuwa donda ndugu ila bado wanajitahidi kupambana nao.

Kadhalika maafisa wa serikali wanaripotiwa kuomba ushirikiano zaidi wa umma katika vita hivyo.Hata hivyo maafisa hao wanazilaumu taasisi zisizo za kiserikali kwa kuongeza chumvi.

Shirika la Transparency International limetoa wito wa mabadiliko ya katiba kufanywa nchini Kenya kwa minajili ya kuyatenga majukumu ya mahakama na serikali.


RTRE
 • Tarehe 09.03.2009
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H8df
 • Tarehe 09.03.2009
 • Mwandishi Thelma Mwadzaya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/H8df
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com