TP Mazembe mabingwa wa Afrika | Michezo | DW | 09.11.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

TP Mazembe mabingwa wa Afrika

Leverkusen na Chelsea kileleni mwa Ligi:

default

Bayer Leverkusen

TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ni mabingwa wapya wa Kombe la klabu bingwa barani Afrika-Wakati Bayer Leverkusen, imefungua mwanya wa pointi 3 kileleni mwa Bundesliga ,Chelsea imepanua mwanya wake hadi pointi 5 katika Premier League baada ya kuipiga kumbo Manchester United kwa bao 1:0.Katika la Liga-Ligi ya Spain, mabingwa FC Barcelona,wamesalia na uongozi wa pointi 1 kileleni .

Tuanze na Ligi mashuhuri barani ulaya:

Bayer Leverkusen sasa inaongoza wazi Bundesliga baada ya kupanua mwanya wake kileleni na mahasimu wake Hamburg na Bremen hadi pointi 3.Leverkusen,isiowahi kutawazwa mabingwa, iliikandika Frankfurt mabao 4:0 ikitia mabao 3 ya kwanza mnamo muda wa dakika 11 tu za mchezo.

Bayer Leverkusen ambayo haikuwahi kushindwa tangu kuanza msimu huu, ilitangulia kwa mabao ya mshambulizi wake Stefan Kiessling,Stefan Reinartz na Toni Kroos kabla Lars Bender, kukamilisha bao lao la 4 katika kipindi cha pili.

Werder Bremen iliopo nafasi ya pili ya ngazi ya Ligi ikiwa na jumla ya pointi 23 ilimdu suluhu tu ya bao 1:1 kati yake na Borussia Dortmund wakati Hamburg pia ikiwa na pointi 23 kama Bremen, iliondoka pia sare kwa kuchapana mabao 2:2 na Hannover.Bremen ilibidi kucheza bila jogoo lao la peru,Claudio Pizzaro.

Mabingwa mara kadhaa wa Ujerumani na Ulaya,Bayern Munich, yaonesha msimu huu unawaendea vibaya.Kwani, baada ya kuzabwa mabao 2 nyumbani na Bordeaux (Bodo) ya Ufaransa kati ya wiki katika kombe la ulaya la Champions League,ilimudu suluhu tu ya bao 1-1 na Schalke.Chipukizi wa miaka 18 wa Schalke ,Joel Matip,nduguye Marvin Matip ,mlinzi wa FC Cologne, ndie alielifumania lango la Munich kwa kichwa na kusawazisha.Ulikuwa mpambano wake wa kwanza kabisa wa Bundesliga. Baba yake Matip ni wa asili ya Kamerun.

Kwa jumla, mtafaruku umezuka katika klabu ya Munich, kutokana na uongozi kukosolewa na beki wao mshahara Philip Lahm.Lahm alikosoa usajili wa wachezaji kuwa si sawa unaegemea ustadi tu wa wachezaji na sio mkakati.

Baada ya kila mechi, yaonesha hatima ya kocha wa Munich, mdachi V an Gaal (Fan Khaal) inajadiliwa na swali linaloulizwa:ni lini atatimuliwa.

Van Gaal, baada ya mpambano wa Jumamosi alieleza hivi:

"Inafadhahisha mno kutotia bao katika kipindi cha pili."Alisema kocha van Gaal kuhusu kipindi ambacho mashambulio ya Munich katika lango la Schalke, yalikuwa makali mno.Hodi -hodi zao nyingi lakini, hazikuitikiwa,kwani Schalke ilitia nta lango lao lisivuje.

Matokeo mengine ya Bundesliga yalikuwa hivi: Borussia Moenchengladbach (Borusia Monshen-gladbakh) ilitoka sare 0:0 na Stuttgart wakati Mainz, ilizima vishindo vya Nuremberg kwa bao 1:0.Mabingwa Wolfsburg ,walitamba nyumbani kwa mabao 2:1 la Hoffenheim.Freiburg, ilitamba mbele ya Bochum kwa mabao 2:1.FC Cologne, ilizima hujuma kali za Hertha Berlin na kwa bao la nahodha wao dakika ya 79 ya mchezo, walitoroka na pointi 3 hadi Cologne.

Ama katika Premier League-Ligi ya Uingereza , changamoto kati ya mahasimu 2 -Manchester United na Chelsea, jana ,ilimalizika kwa ushindi wa bao 1:0 wa Chelsea.Kwa ushindi huo, Chelsea imepanua mwanya wake kileleni kati yake na Manu kwa pointi 5. Bao la kichwa la dakika ya 76 ya mchezo la John Terry, liliamua ubishi kati yao na sasa Chelse, ina pointi 30-tano zaidi kuliko Arsenal walioitandika Wolverhampton mabao 4-1.

Katika la Liga-Ligi ya Spain , mabingwa FC Barcelona, wameseleleza mwanya wao wa pointi 1 kileleni mbele ya Real Madrid,mahasimu wao.Pedro alitia mabao 2 kabla Thiery Henry kutia bao lake la kwanza msimu huu kukamilisha ushuindi wa mabao 4-2 dhidi ya Real Mallorca. Real Madrid, iliizaba Atletico Madrid mabao 3:0. Sevilla imen'gan'gania nafasi ya 3 kwa ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Villareal.

Baada ya firimbi ya mwisho kulia katika finali ya kombe la klabu bingwa barani Afrika,ilikuwa "asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo-mkutano mitaani mjini Lumbubashi". TP Mazembe imetawazwa tena mabingwa wa Afrika.Zikisalia dakika 17 kabla ya firimbi ya mwisho kulia, Heartland ya Nigeria, ilitia bao katika lango lao wenyewe na kuwapa sadaka wenyeji wao .Timu hizi 2 zilimalizana sare mabao 2:2 kwavile Heartland ilishinda duru ya kwanza mjini Oweri jumapili iliotangulia .Halafu mlinzi wa Heartland Victor Ezuruike alilifumania lango lake mwenywe na kuwafanya mashabiki 35,000 katika kenya Stadium,mjini Lumbubashi kuanza kushangiria.

TP mazembe ,ilitwaa kombe hili mara ya kwanza 1968 na ikalitwaa tena na kuwa timu ya kwanza kuvaa taji mara 2 mfululizo.

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com