″Timu hiyo inasikitisha″ | Magazetini | DW | 22.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Timu hiyo inasikitisha"

Wahariri wa magazeti leo hii wanazingatia siasa za ndani ikiwa ni miaka miwili baada ya serikali ya mseto ya Ujerumani kuanza kipindi chake cha kazi, wakati ambapo nusu yake kipindi chake kimepita.

Vyama tawala vya Berlin

Vyama tawala vya Berlin

Kwanza ni gazeti la “Neues Deutschland” ambalo linatumia lugha ya mchezo wa soka likiandika:


“Kipenga cha kipindi cha mapumziko kimesikika na serikali hii inafanya bidii kubwa kutoa picha ya timu iliyofanikiwa. Lakini baada ya miaka miwili ya kupiga chenga pale pale ilipo, timu hii kweli inasikitisha. Mijadala mirefu mno, makubaliano yasiyo na maana, maamuzi yaliyoahirishwa na mazungumzo yaliyoendelea mpaka usiku bila ya kuleta suluhisho kweli hayakuweza kuwavutia “watangazaji” wa mechi hiyo ambao juu ya hayo wanakasirika kutokana na sheria mpya zinazowaathiri.”


Vyama viwili vikubwa vya Ujerumani ambavyo zamani vilikuwa washindani viliungana katika serikali hii, chama cha kihafidhina cha Christian Demokrats CDU, na chama cha kijamii cha Social Demokrats, SDP. Mhariri wa gazeti la “Lübecker Nachrichten” anaangalia kwa nini vyama kivi haviwezi kuelewana. Ameandika:


“Tatizo kubwa la serikali hiyo ni kwamba pande hizo mbili zinapata sifa tofauti. Chama cha CDU kinajisikia kama kimeimarika sana kuwatukana wenzao wa SPD. Wanasiasa wa chama cha Social Demokrats kwa sasa wanasumbuliwa sana na matokeo mabaya ya kura ya maoni. Kwa hivyo, chama hiki sasa kinajaribu kujipatia sifa kwa kugombana na mshirika wake. Lakini hiyo pia haikisaidii chama hiki, tukiwaamini wachunguzi wa maoni. Kwa bahati mbaya, siku za tija za serikali hii zimepita.”


Suala moja lililozusha mvutano kati ya vyama vya CDU na SPD ni sera za kuelekea China baada ya Kansela Angela Merkel wa chama cha CDU alipopokea kiongozi wa kidini wa Tibet, Dalai Lama, na hivyo kusababisha mpasuko fulani na China. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier ambaye ni wa chama cha SPD alimkosoa Kansela Merkel kwa hatua hiyo. Hili hapa ni gazeti la “Kieler Nachrichten” juu ya mgogoro huu:

“Chini ya Makansela wa zamani Helmut Kohl na Gerhard Schröber, Ujerumani ilikuwa rafiku wa karibu wa China. Bila ya kujali ukiukaji wa haki za binadamu, Makansela hao wa Ujerumani waliinamisha kichwa mbele ya viongozi wa China. Waziri wa nje Frank-Walter Steinmeier ambaye anatarajiwa kuwa mgombea wa kiti cha Kansela kwa upande wa SPD katika uchaguzi ujao anapaswa kujitenga na sera za kansela wa zamani Gerhard Schröder. Chama cha SPD kinapigania kuwasaida wanaokandamizwa, ikiwa ndani ya Ujerumani au nje. Wapigaji kura hawatapendelea sera za kujifanyia rafiki wa Hu Jintao wa China wala wa Vladimir Putin wa Urusi.

 • Tarehe 22.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CS24
 • Tarehe 22.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CS24
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com