Timu 9 mbioni kuwania ubingwa Bundesliga | Michezo | DW | 21.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Timu 9 mbioni kuwania ubingwa Bundesliga

Ligi ya Ujerumani Bundesliga katika mchezo wake wa nane imeingia katika msongamano wa timu kuelekea kileleni baada ya timu tisa kupishana kwa pointi mbili tu kutoka timu inayoongoza kileleni.

Mchezo wa  nane wa  Bundesliga umetoa  matokeo yasiyoonesha mwelekeo  halisi wa  ligi  hiyo baada  ya  vigogo  wa  ligi  kupokea vipigo na  kushikwa  shati , hali inayoelezea  ugumu  wa  ligi  msimu huu. Baada  ya  kutoka  sare mara  tatu  mfululizo makamu  bingwa Borussia  Dortmund ilijikakamua  na  kupata  ushindi  wa  kibarua wa bao 1-0 dhidi  ya Borussia Moenchengladbach siku  ya  Jumamosi na  kumpa kocha wa  Dortmund pamoja  na  wachezaji  nafasi  ya kupumua baada  ya  ukosoaji  mkubwa  dhidi  ya  kikosi  hicho jinsi kinavyocheza. Dortmund ilitangaza  mwanzoni  mwa  msimu  kuwa mara  hii  ina nia  ya  kulinyakua  taji  la  ubingwa  wa  Bundesliga. Lakini  hali  yake  ya  kusuasua  imeweka  kiwingu katika  dhamira hiyo.

Deutschland Borussia Dortmund gegen Borussia Mönchengladbach (Getty Images/Bongarts/D. Mouhtaropoulos)

Marco Reus nahodha wa Borussia Dortmund

Nahodha wa  Borussia  Dortmund  Marco Reus  anakiri kuwa ushindi  huo umeleta ahueni  katika  kikosi.

"Baada  ya  wiki tatu, nne ambamo tulipata  matokeo ya  sare, shinikizo bila  shaka lilikuwapo, katika mchezo wetu huu. Tumeshuhudia  pia, kwamba si kwa bahati kuwapo katika  nafasi za juu. Naamini kwamba  mchezo huu ulikuwa na tofauti ndogo sana kwa kila  upande  na  ungeweza pia  kwenda upande mwingine. Lakini mara hii  bahati kidogo  ilikuwa  upande wetu na leo tumefaidika kutoka na jinsi tulivyoweka  bidii, na  kwamba  hatukukata tamaa, tuliendelea  kujiamini na mwishowe tumeshinda."

Mchezaji  wa  kati  wa  Borussia  Moenchengladbach  Christoph Krammer, lakini anasikitika kwa  timu  yake  kukosa  ushindi  licha ya  juhudi kubwa , na  pia  akilamikia  maamuzi  kwamba  wakati mwingine  yalikuwa  yakienda dhidi  yao.

"Tulipata  nafasi  nyingi sana, lakini  kila  mara  kulikuwa  na  mguu wa  mchezaji wa  Dortmund katika  sekunde ya  mwisho. Si  makosa ya  kutoweka  mbinyo zaidi ama  kupoteza umakini, hilo ni suala mara  nyingine la  bahati  tu ama  mkosi. Na katika sehemu  nyingine, ilikuwa  ni  kutokana  na uamuzi unaoweza kwenda huku ama  kule, ama  pengine penalti ama sio. Pambano la  Hummels dhidi  ya Hermann, nafikiri, inawezekana  bila  shaka ikawa penalti. Lakini hatuwezi kutoa  lawama nyingi. Tulipata nafasi saba, ama nane nzuri sana dhidi ya  Dortmund, ambazo tungeweza kirahisi kuuweka mpira wavuni, kwa  kuwa  nafasi zilikuwa nyingi za kuweza  kushinda mchezo  huo."

1. Bundesliga | Eintracht Frankfurt - Borussia Mönchengladbach (picture-alliance/AP Photo/M. Probst)

Christoph Kramer wa Borussia Moenchengladbach

Mbali  ya  vuta nikuvute  hiyo  kati ya  Borussia  Moenchengladbach ambayo  inashilikilia  bado  nafasi  ya  uongozi  wa  ligi kwa  kuwa na  pointi 16, dhidi  ya  Borussia  Dortmund  yenye  pointi  15 , lakini pambano  lililokuwa  gumzo  ni  kati  ya  mabingwa  watetezi  Bayern Munich  dhidi  ya  FC  Augsburg. Mchezo  huo  uliishia  sare  ya mabao 2-2 na  pia  kusababisha  ukosoaji  dhidi  ya  kocha  Nico Kovac. Ni  vipi Augsburg inayojikuta  hivi  sasa  katika  nafasi  ya 16 ya  msimamo wa ligi  na  ikiwa  na  pointi 6 tu baada ya  michezo minane imeweza  kuwasimamisha  mabingwa watetezi, anafafanua hapa  mchezaji Stephan Lightsteiner wa Augusburg.

"Nafikiri , tumepambana  kuzuwia kwa  mikono  na  miguu leo. Mlinda mlango Koubek alifanya kazi  nzuri sana leo. Na  pia  tuliweza  kwa upande  wa  ulinzi kufanya  vizuri.  Bila  shaka  si rahisi  dhidi  ya Bayern kujilinda  hadi  mwisho. Ni kweli  kwamba  walituachia nafasi ya  kupumua na  hadi  mwisho  tulijiamini na  kupata bao na  kupata sare  ya  mabao 2-2.

Bayer Leverkusen ilishangazwa  na  Eintracht  Frankfurt  kwa  kipigo cha  mabao 3-0 siku  ya  Ijumaa  , na  jana  Schalke 04 ilishindwa kuchupa  hadi  nafasi  ya  kwanza  pale  walipoduwazwa  kwa mabao 2-0 dhidi  ya  TSG Hoffenheim. Nayo FC Kolon jana imechupa kutoka  nafasi ya  17, hadi  nafasi  ya  15 , baada  ya kuikandika  SC Paderborn 07 kwa  mabao 3-0 nyumbani  na kujikusanyia jumla ya  pointi 7.

Deutschland Bundesliga 1. FC Köln - SC Paderborn 07 | Tor Terodde (Imago-Images/M. Müller)

Wachezaji wa FC Kolon wakifurahia bao dhidi ya SC Paderborn

Hata  hivyo msuguano kuelekea  kileleni  mwa  msimamo  wa  ligi  ni mkubwa, ambapo timu tisa zina uwezo  wa  kukalia  kiti  cha  usukani katika  mchezo  wa  9  wa  Bundesliga. Timu 4 zinafungana  katika pointi 4, timu 3 zina pointi 15 na  timu  mbili zina  pointi 16, tofauti ikiwa  pointi 2 kati ya  timu  ya  tisa Bayer Leverkusen  na  timu inayoshikilia  nafasi  ya  kwanza Borussia  Moenchengladbach yenye  pointi 16.