Tillerson aanza ziara ya bara la Afrika
8 Machi 2018Rais wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki amepuuzia tukio hilo na kusema ni "mambo yaliyopita". Tillerson hata hivyo amezitahadharisha nchi za Afrika kutotupa uhuru wao kwa kukubali mikopo kutoka China.
Mapema mwaka huu , rais wa Marekani Donald Trump alisababisha hasira katika bara hilo baada ya kuripotiwa akisema kwamba baadhi ya nchi za Afrika ni kama zimo katika shimo lenye uvundo, na kusababisha mataifa kadhaa kuwaita mabalozi wa marekani katika nchi zao kupta ufafanuzi na kudai kuombwa msamaha.
Kumekuwa na uvumi kwamba Rex Tillerson anaweza kukabiliwa na uhasama katika ziara yake ya Afrika kutokana na matamshi hayo, lakini mwenyekiti wa halmashauri ya Umoja wa Afrika Moussa Faki amepuuzia maswali kuhusu suala hilo katika mkutano na waandishi habari akiwa pamoja na waziri Tillerson mjini Addis Ababa leo Alhamis.
"Naamini kwamba tukio hilo kuhusiana na matamshi ya rais Trump kuhusu Afrika limepita. Naamini kwamba ziara hii leo ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Tillerson ni uthibitisho wa uhusiano baina ya Afrika na Marekani."
Tillerson atangaza misaada kwa Afrika
Ziara hiyo ya Afrika , ambayo pia inajumuisha Chad, Djibouti, Kenya na Nigeria ni ya kwanza kufanywa na Tillerson tangu alipokuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, na alitangaza zaidi ya dola nusu bilioni za misaada kabla ya kuanza ziara hiyo. Tillerson amesema Marekani inatoa msaada wa kiutu , kupambana na njaa na ukame pamoja na hali ya kutokuwa na uhakika wa chakula.
Akiwa katika mji mkuu wa Ethiopia leo, Tillerson amezungumzia kuhusu hali ya China kusambaa katika bara hilo, akizitahadharisha nchi hizo kutotupa uhuru wao.
"Tuna shuhudia kauli mbiu ambayo China inaifuata. Hawaleti uwezo wa ujenzi wa nafasi za kazi, hawaleti mipango halisi ya mafunzo ambayo itawawezesha Waafrika kushiriki zaidi katika maisha ya baadaye, na mara nyingi utaratibu wa utoaji wa mikopo uko katika njia kwamba nchi , inapopata matatizo kifedha, inapoteza uwezo wa kudhibiti miundo mbinu yake ama maliasili zake kutokana na kushindwa kulipa."
Tillerson amesema Marekani haijaribu kuondoa uwekezaji wa China kutoka bara la Afrika , lakini amesema , "ni muhimu kwa nchi za Afrika kutafakari kwa uangalifu masharti ya uwekezaji huo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / rtre
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman