Tikiti za pigano la Mayweather na Pacquiao zanunuliwa zote | Michezo | DW | 24.04.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Tikiti za pigano la Mayweather na Pacquiao zanunuliwa zote

Wasimamizi wa pigano kubwa kabisa kati ya Manny Pacquiao na Floyd Mayweather wamechukua hatua isiyo ya kawaida kwa kutoza ada ya kiingilio wakati wa kupima uzani wa mabondia hao.

Hii ni baada ya tikiti za pigano lenyewe kuisa zote punde baada ya kuanza kuuzwa rasmi. Tikiti za shughuli hiyo ya kupima uzani mnamo Mei mosi, pia katika ukumbi wa Grand Garden Arena ndani ya hoteli ya MGM mjini Las Vegas, zimeanza kuuzwa leo Ijumaa na zinagharimu dola kumi, kwa kila tikiti.

Chini ya sheria za jimbo la Arizona, shughuli za mabondia kupimwa uzani hufanyika bila malipo kwa umma. Lakini mapromota wanatumai kuwa kwa kutoza ada ya kiingilio, itasaidia kuwazuia maelfu ya mashabiki wa masumbwi dhidi ya kukita kambi usiku kucha nje ya hoteli ya MGM ili kujaribu kupata tikiti. Mayweather dhidi ya Pacquiao ni tamasa kubwa zaidi la ndondi katika historia ya karibuni na litatumika kuamua ni nani bondia bora zaidi wa enzi yao.

Mabondia wote wanatarajiwa kutia kibindoni zaidi ya dola milioni 100 kutokana na pigano hilo la uzani wa welter huku asilimia 60 ya kitita hicho ikimwendea Mayweather, naye Pacquiao akiridhika na asilimia 40.

Lakini wakati tukisubiri pigano hilo la Mei 2, yapo mengi tu yanayojitokeza. Sasa, imebainika kuwa Manny Pacquiao haipendi tena hoteli ambako kutaandaliwa pigano lake na Mayweather Jr. Mfilipino huyo anapanga kususia sherehe za Jumanne katika hoteli ya MGM Grand zinazoashiria kuwasili rasmi kwa mabondia, hafla ambayo imekuwa sehemu ya utamaduni wa hoteli hiyo wakati wa mapigano makubwa. Pacquiao anaishi katika hoteli nyingine mjini Las Vegas na ataandaa sherehe za baada ya pigano katika hoteli nyingine inayofahamika kama Wynn. Ni kwa nini haitaki MGM? Msimamizi wake Bob Arum – ambaye amekuwa katika mgogoro na hoteli hiyo kuhusiana na mauzo ya tikiti – amesema Pacquiao atakwenda tu katika hoteli ya MGM kwa kikao cha mwisho cha waandishi wa habari kabla ya pigano, wakati wa kupima uzani na siku ya pigano lenyewe.

Hoteli ya MGM ndipo mahala ambapo Pacquiao ameshinda mapigano yake makubwa, yakiwemo didi ya Oscar De La Hoya, Miguel Cotto na Ricky Hatton. Pigano dhidi ya Mayweather litakuwa lake la 12 katika hoteli hiyo ambayo ni maarufu mjini Las Vegas, kwa kuandaa mapingano makubwa kabisa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AP/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba