1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May apeleka kilio chake Brussels

Saumu Mwasimba
13 Desemba 2018

Baada ya kuufanikiwa kuungwa mkono na kuepuka kuangushwa katika kura ya kutokuwa na imani nae bungeni,May anajiandaa kuomba msaada mkubwa Umoja wa Ulaya wa kupata hakikisho juu ya mpango wake wa Brexit

https://p.dw.com/p/3A0kf
Theresa May
Picha: picture-alliance/empics

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May yuko Brussels atakakoshiriki mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja wa Ulaya kutafuta msaada na hakikisho kuhusu mpango wake wa kuachana na Umoja wa Ulaya.Safari hii ya May inakuja baada ya jana kuepuka kuangushwa katika kura ya kutokuwa na imani na uongozi wake. Nchi za Umoja wa Ulaya zimefurahishwa na matokeo ya kura hiyo  ingawa nchini Uingereza kwenyewe mgawanyiko unaonekana kuongezeka bungeni.

Theresa May ameshusha pumzi baada ya kuepuka kuangushwa katika kura ya kutokuwa na imani nae,leo hii anaelekea mjini Brussels kutakakofanyika mkutano wa siku mbili wa viongozi 28 wa Umoja wa Ulaya,na Brexit  ndio suala litakalohodhi katika kikao hicho. Dhamira kubwa ya waziri mkuu huyo wa Uingereza ni kutaka kuwaomba viongozi wa Umoja wa Ulaya kumsaidia katika mpango wake wa Brexit.Anataka apewe hakikisho litakalomuwezesha kulishawishi bunge la nchi yake mjini London ambalo linautilia mashaka makubwa mpango wake huo.Lakini Umoja wa Ulaya unashikilia kwamba hakuna kinachoweza kubadilishwa kwa uhakika katika mpango huo wa kisheria. Pamoja na hayo viongozi mbali mbali wa Umoja wa Ulaya wameonesha kufurahishwa na hatua ya wabunge waliopiga kura ya kuwa na imani na waziri mkuu wao Theresa May katika mchakato uliofanyika jana. Hivi sasa May anakutana na mwenzake wa Ireland Leo Varadkra mjini Brussels kabla ya mkutano huo wa kilele.

Brüssel Theresa May, Premierministerin Großbritannien
Picha: Reuters/D. Martinez

 Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amesema ameshusha pumzi kuona kwamba chama cha Conserative kimeepuka kuuanzisha mgogoro kamili katika mchakato wa Brexit lakini pia Heiko Maas ameonesha kwamba bado kuna nafasi ndogo ya Uingereza kufikia maridhiano kuhusiana na mpango wake wa kuachana na Umoja wa Ulaya. Waziri Maas alipoulizwa kitu gani kinachoweza kufanywa ili Uingereza iweze kupata idhini bila ya majadiliano mapya au kufanyika mabadiliko kwenye mpango wa Brexit alijibu kwamba uamuzi wa mwisho wanao wenyewe Waingereza ndio wanaotakiwa kuuambia Umoja wa Ulaya kuhusiana na hilo kwasababu ikiwa Umoja wa Ulaya umeshatowa mapendekezo hivi sasa hakuna anayeweza kusema chochote kutokana na mkanganyiko uliopo London kwa hivi sasa.

Taarifa ya Umoja wa Ulaya ambayo tayari imeshaandaliwa na imeonekana na shirika la habari la Reuters inaonesha kutoa msisitizo kwamba Umoja huo unapendelea kuwa na mkataba mpya na Uingereza  juu vipengee vinavyoleta utata lakini nchi nyingi za Umoja huo wa Ulaya hazijakubaliana kuhusu mkataba huo kufikia leo asubuhi na wanadiplomasia mjini Brussels wanatarajia kuona mkataba huo unabadilishwa.Inatajwa kwamba inaelekea Umoja huo huenda ukawa tayari kumpa hakikisho zaidi Theresa May mwezi Januari katika wakati ambapo siku ya Uingereza ya kuanza kuutekeleza mpango wa Brexit ukiwa ni Tarehe 29 Marchi.Mbunge anayeunga mkono Brexit kutoka chama cha Conservative Jacob Rees-Mogg amesema hivi:

"Waziri mkuu lazima atambue kwamba chini ya vipengele vyote vya katiba anatakiwa kufikia uamuzi wa kwenda kumuona malkia haraka na kujiuzulu na nitakwambia kwanini. Kikatiba ikiwa waziri mkuu hawezi kuendesha shughuli zake kupitia bunge na jumatatu waziri huyo akasimama kukiri kwamba anajua atashindwa kwenye bungeni kuhusu mpango wake wa Brexit  na kwahivyo akaamua kuiakhirisha kura hiyo.Na baadae akaja kutambua kwamba wengi wa wabunge kutoka chama chake wamepiga kura ya kuonesha hawana imani nae,basi ni wazi hana imani ya bunge.Anapaswa kumpisha mwingine mwenye imani ya bunge.

Großbritannien Zeitungen nach Misstrauensvotum
Picha: DW/B. Wesel

Gazeti la Daily Mirror limeandika  kwamba May amevurugwa na anakabiliwa na vikwazo vigumu zaidi katika mpango wa Brexit licha ya ushindi wake. Gazeti hilo linasema amepata tiketi ya kubakia kwa ajili ya kukiona kifo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo