1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theluthi ya chakula cha dunia hutupwa kila mwaka

Admin.WagnerD12 Septemba 2013

Theluthi moja ya chakula kinachozalishwa duniani kila mwaka hutupwa, na kuugharimu uchumi wa dunia karibu euro bilioni 570 kila mwaka, limesema shirika la chakula la Umoja wa Mataifa FAO.

https://p.dw.com/p/19gPv
FAO imesema tani bilioni 1.3 za chakula hupotea au kutupwa kila mwaka, huku watu milioni 870 wakishinda na njaa duniani.
FAO imesema tani bilioni 1.3 za chakula hupotea au kutupwa kila mwaka, huku watu milioni 870 wakishinda na njaa duniani.Picha: picture-alliance/dpa

Katika ripoti yake iliyotolewa mjini Rome nchini Italia siku ya Jumatano, FAO imesema uharibifu huu mkubwa wa chakula hauathiri tu uchumi wa dunia, bali mazingira pia.

Wakati wakifanya manunuzi yao ya kila siku, walaji wengi hawajui ni kiasi gani cha chakula hutupwa. Lakini mamilioni ya tani za mchele, matunda na mbogamboga huishia katika mapipa ya taka kila mwaka, limesema shirika la FAO lenye makao yake mjini Rome Italia. Kwa ujumla, FAO inasema karibu tani bilioni 1.3 za chakula zinaharibiwa ambako bara la Asia ndiyo linaongoza katika uharibifu huu.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva.
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva.Picha: DW/R. Belincanta

'Ni tukio la kushtusha'
Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Jose Granziano da Silva, aliwaambia waandishi wa habari mjini Rome, kuwa thamani ya chakula kinachoharibiwa ni sawa na pato la ndani la jumla la Usiwisi, na kuongeza kuwa wakati kiasi hicho cha chakula hupotea kutokana na matendo yasiyofaa, watu milioni 870 wanashinda na njaa kila siku. Achim Steiner, mkuu wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa, UNEP, aliuelezea muelekeo huu kama tukio la kustusha.

Katika mataifa yanayoendelea, ripoti hiyo imebainisha kuwa chakula kinapotea kutokana na mavuno yasiyo na ufanisi au mazingira duni ya uhifadhi, wakati katika mataifa tajiri matunda na mbogamboga hutupwa kutokana na sababu za muonekano ambao hauwapendezi wanunuzi, au rangi, au chakula kinatupwa kutokana na ununuzi wa kupita kiasi.

FAO ilisema kila mwaka, chakula kinachozalishwa na kutoliwa kinanyonya kiwango cha maji sawa na kinachotiririka katika mto Volga nchini Urusi, na chakula hicho kinahusika na tani bilioni 3.3 za gesi chafu inayoingia katika anga ya sayari. Mkuu wa UNEP, Achim Steiner, alisema kuondoa uharibu wa chakula kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza baa la njaa, na kutoa wito kwa kila mtu kuchukua hatua kukabiliana na tatizo hili.

Bara la Asia laongoza kwa kuharibu chakula
Ripoti hiyo ililinyooshea kidole hasa bara la Asia, ikisema kuwa wastani wa kilo 100 za matunda kwa kila mtu zinatupwa kila mwaka, katika mataifa yalioendelea kiviwanda barani humo, yakiwemo China, Japan na Korea Kusini. Ripoti hiyo ilikadiria kuwa kanda hiyo inaharibu kilo 80 za nafaka - hasa mchele kwa kila mtu, na kuonya kuwa kilimo cha mchele kinatoa kiwango kikubwa cha gesi ya kaboni, na kimekuwa mmoja ya vyanzo vikubwa vya uchafuzi wa mazingira.

Kilimo cha mchele kinaelezwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.
Kilimo cha mchele kinaelezwa kuwa chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.Picha: Getty Images

Maeneo mengine yaliyobainishwa katika ripoti hiyo yanayochangia uharibifu na kuathiri mazingira, ni sekta za nyama Amerika kaskazini na Kusini, na pia uharibifu wa matunda barani Asia, Ulaya na Amerika Kusini. Chakula kinachozalishwa lakini hakiliwi kinatumia asilimia 30 ya ardhi ya kilimo duniani, imesema ripoti hiyo.

Nini kifanyike?
Ushauri juu ya kupunguza uharibifu wa chakula unahusisha kupanga mapema safari za manunuzi, na kutonunua zaidi ya kile kinachohitajika, na pia kutoa chakula cha ziada kulisha wanajamii walio katika hatari zaidi, na pia kutumia chakula ambacho hakifai tena kuliwa na watu kulisha mifugo. FAO pia ilisisitiza umuhimu wa urejelezaji wa chakula kisichotumiwa, ikisema kuwa chakula kisicholiwa na kuoza kinazalisha gesi kubwa ya methane, ambayo ni hatari sana.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe,dpa,kna, afpd
Mhariri: Mohammed Khelef