1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Thamani ya sarafu ya Lira yaanguka vibaya, Uturuki

Amina Mjahid
13 Agosti 2018

Benki kuu ya Uturuki imetangaza mikakati yake ya kuzisaidia benki nchini humo kupambana na ukwasi wakati taifa hilo likikumbana na mgogoro wa kifedha pamoja na ule wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Marekani. 

https://p.dw.com/p/3345X
Türkei, Istanbul: Finanzminister  Berat Albayrak  hält Ansprache
Picha: picture-alliance/M. Alkac

Mgogoro huo wa kiuchumi nchini Uturuki ulioanzishwa na wasiwasi juu ya sera za kiuchumi za rais Recep Tayyip Erdogan, biashara pamoja na mgogoro wa kidiplomasia kati ya Uturuki na Marekani umesababisha thamani ya sarafu ya Uturuki ya Lira kuanguka katika wiki zilizopita na kuanguka zaidi kwa asilimia nyengine 7 hii leo wakati mikakati ya benki ya dunia ikishindwa kurejesha imani ya waekezaji. 

Türkei Börse in Istanbul
Picha inayoonesha thamani ya sarafu ya Lira katika soko la hisa mjini Istanbul, Uturuki Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Sarafu hiyo imeanguka kwa kiwango cha chini zaidi cha lira 7.23 kwa dola  hapo jana jioni, baada ya rais Erdogan katika mfululizo wa hotuba zake wiki nzima kutoonesha dalili yoyote ya kurejea nyuma katika vita vyake vya kidiplomasia na Marekani mwanachama wa Jumuiya ya kujihami ya  NATO.

Erdogan hata hivyo ameondoa uwezekano wa kuwa na viwango vikubwa vya riba ambavyo wanauchumi wanasema vinahitajika na ni muhimu katika kuimarisha thamani ya lira. Rais huyo wa Uturuki pia ametishia kutafuta washirika wapya na kuonya kuwepo kwa mikakati mikali zaidi iwapo biashara zitaondoa safaru za kigeni katika mabenki. 

Wataalamu wa kiuchumi wasema matamshi ya rais Erdogan hayasaidii kupata suluhisho ya matatizo yaliopo.

Simon Derrick, mtaalamu wa sarafu katika kampuni moja ya BNY Mellon, amesema kutokana na kutopandishwa viwango vya riba ni vigumu kuangalia matamshi ya rais kama suluhisho kwa matatizo ya kiuchumi yaliopo lakini ni hatua ya muda tu ya kupoza mambo.

Mapema hii leo taarifa ya  benki kuu ya Uturuki ilisema  kwamba kuna mipango maalum iliowekwa ili kutoa ukwasi kwa mabenki nchini humo. Hatua hiyo inanuiwa kuupa unafuu mfumo ya kifedha na kufuta wasiwasi wa matatizo katika mabenki  ili kuwawezesha kuendelea kutoa mikopo kwa watu na wafanyabiashara.

Türkei, Trabzon: Erdogan hält eine Rede
Rais Tayyip Erdogan akiwahutubia wafuasi wake mjini Trabzon, UturukiPicha: picture-alliance/AP Photo

Kwa kawaida wakati wa mashaka ya kiuchumi au mgogoro wa kiuchumi mabenki huacha kukopeshana na mara moja hatua kama hizi husababisha kuporomoka kwa mabenki hayo. Kwa mwaka huu pekee Lira imeanguka kwa karibu asilimia 45.

Aidha mgogoro wa Uturuki na Marekani unaendelea kutokana na kuwekwa kizuizini mchungaji wa kimarekani aliefunguliwa mashitaka ya udukuzi na madai mengine ya kigaidi. Marekani imejibu kwa kuwawekea vikwazo vya kiuchumi mawaziri wawili nchini Uturuki pamoja na  kuongeza ushuru wa bidhaa za chuma na bati kutoka Uturuki.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman