Tetemeko lengine laikumba Japan | Masuala ya Jamii | DW | 08.04.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Tetemeko lengine laikumba Japan

Tetemeko lingine la ardhi lenye kipimo cha 7.4 limeikumba Japan na kusababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa na pia kuathiri kituo kingine cha nyuklia cha Onagawa.

default

Kiwanda cha nyuklia cha Onagawa

Tetemeko hilo la ardhi lilisababisha kukatika kwa umeme katika eneo kubwa la kaskazini mwa Japan na pia kulazimisha mitambo ya kupoozea hewa katika viwanda vitatu vya nyuklia kuwasha umeme wake wa dharura na pia kaya zaidi ya milioni 3.3 kubakia bila ya umeme jana usiku.

Maafisa nchini humo wanasema tetemeko hilo lililotokea jana usiku lilikuwa ni moja wapo ya matetemeko mabaya kuwahi kuikumba nchi hiyo tangu ilipokumbwa na janga baya zaidi la tetemeko la ardhi na tsunami karibu wiki nne zilizopita.

Mara tu baada ya kutokea kwa tetemeko hilo, Mamlaka ya Utabiri wa hali ya hewa ya Japan ilitoa tahadhari ya kutokea kwa Tsunami, kwa kuonya kwamba  mawimbi makubwa yenye urefu wa mita sita yatalikumba eneo hilo.

Hata hivyo tangazo hilo liliondolewa baada ya dakika 83 toka kutolewa.

Tetemeko hilo pia limesababisha hofu kwa wakaazi wa eneo la kaskazini magharibi mwa Japan, ambapo jana usiku wakazi wa mji wa Kitakami walimiminika katika maduka yanayouza bidhaa usiku kununua vyakula, maji na betri kwa wingi, ili kuweza kuweka tena akiba.

Katika hatua nyingine waendeshaji wa mtambo wa nyuklia wa Onagawa, wamegundua kuvuja kwa kiasi kidogo cha maji katika maeneo matano ya kiwanda, ikiwemo ndani ya majengo, baada ya kutokea kwa tetemeko hilo la jana usiku.

Kampuni ya umeme ya Tohoku ambayo inaendesha kiwanda hicho kilichoko katika mji wa Miyagi imesema maji yalivuja na kumwagika sakafuni kutoka katika mitambo ya vinu vitatu.

Kampuni hiyo ya umeme imekuwa ikiendeleza juhudi za kuchunguza madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo la jana, lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyoonekana katika kupanda ama kushuka kwa viwango vya mionzi katika mtambo huo.

Kiwanda hicho kilikuwa kimesimamisha shughuli zake, tangu kutokea tetemeko baya la ardhi la Machi 11, ambalo liliathiri vibaya kiwanda cha nyuklia cha Fukushima.

Katika hatua nyingine China imesema ina wasiwasi na hatua ya Japan kuruhusu maji machafu yaliyotoka katika mitambo ya nyuklia iliyoathiriwa na tetemeko la ardhi kuingia baharini. na kuitaka nchi hiyo kulinda mazingira ya bahari.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton anaweza kuyatembelea maeneo ya kaskazini mashariki mwa Japan, ambayo yamekumbwa na tetemeko la ardhi baadaye mwezi huu.

Anatarajiwa kuitembelea nchi hiyo Aprili 17 hadi 18, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa pande mbili, hususan kufuatia janga la tetemeko la ardhi na tsunami lililoikumba Japan mwezi uliopita.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa,afp)

Mhariri:Aboubakary Liongo

 • Tarehe 08.04.2011
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10pkY
 • Tarehe 08.04.2011
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10pkY
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com