1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tennis yakumbwa na madai ya udanganyifu

18 Januari 2016

Mchezo wa Tennis ulimwenguni umekumbwa na madai kuwa viongozi wa mchezo huo wameshindwa kukabiliana na matukio ya kupanga matokeo ya mechi

https://p.dw.com/p/1HfVY
Symbolbild Tennis ATP World Tour
Picha: picture-alliance/dpa/J.C. Hidalgo

Hayo yamejiri wakati tu mashindano ya Australian Open, kinyang'anyiro cha kwanza cha grand slam mwaka huu, kikianza mjini Melbourne.

Maafisa wa Tennis wamekanusha ripoti za shirika la habari la BBC na mtandao wa BuzzFeed News, ambazo zilisema kuwa wachezaji 16 ambao wamejumuishwa katika orodha ya wachezaji 50 bora na walitambuliwa na maafisa wanaosimia uadilifu katika mchezo huo, Tennis Integrity Unit – TIU kuhusiana na tuhuma kuwa walishindwa mechi zao kwa hiari katika muongo mmoja uliopita.

Wanane kati ya wachezaji hao wanashiriki katika mashindano ya Australian Open. Madai hayo yanayofuata kashfa za rushwa katika michezo ya Kandanda na riadha ulimwenguni, yamezusha hisia tofauti huku wachezaji wakielezea kushangazwa kwao akiwemo Serena Williams mchezaji anayeorodheshwa namba moja ulimwenguni.

Ripoti hizo zinaongeza kuwa wachezaji hao wote 16, wakiwemo washindi wa mataji ya grand slam, waliruhusiwa kuendelea kushiriki mashindanoni. Mkurugenzi mkuu wa uadilifu katika TIU Nigel Willerton amesema hawezi kuzungumza ikiwa wachezaji wowote wanaoshiriki katika mashindano hayo wanafanyiwa uchunguzi, akisema haitakuwa vyema kulizungumzia hilo.

BBC na BuzzFeed News wamesema hawangeweza kuwataja wachezaji wowote kwa sababu bila kuona simu zao, rekodi za benki na kompyuta ni vigmu kubainisha ikiwa walishiriki katika kupanga matokeo ya michuano.

Chris Kermode mwenyemiti wa Chama cha Wachezaji wa Tennis kwa Wanaume – ATP amekanusha kuwa matokeo ya uchunguzi huwa yafanichwa. Kermode aidha amesema inasikitisha kuwa habari hizi zimetolewa katika wakati ambapo mashindano makubwa yameanza

Aliyekuwa mchezaji nambari moja ulimwenguni katika mchezo huo Muingereza Andrew Castle pia ametoa atoa sauti yake kuhusiana na habari hizi akisema anaona namna kunaweza kuwa na majaribu ya kupanga matokeo ya mechi katika mashindano ya tennis ya viwango vya chini

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman