TEHRAN:Rais wa Iran asema katu mpango wake wa Kinuklia hausimami | Habari za Ulimwengu | DW | 26.02.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

TEHRAN:Rais wa Iran asema katu mpango wake wa Kinuklia hausimami

Rais wa Iran Mahmoud Ahmedinejad amesema nchi yake haitorudi nyuma juu ya mpango wake wa Kinuklia unaozozaniwa.Rais Ahmedinejad ameufananisha mpango wake wa Kinuklia na treni isiyokuwa na breki.

Awali naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran alisema wako tayari kwa lolote na nchi za magharibi hata ikiwa ni kuingia katika vita.

Matamshi hayo makali kutoka upande wa Iran yamekuja kabla ya mkutano baina ya wawakilishi wa nchi tano wanachama wa kudumu katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani utakaofanyika hii leo mjini London kujadili hatua zaidi zitakazochukuliwa dhidi ya Iran.

Wasiwasi pia umezuka baada ya Iran kurusha roketi yake ya kwanza kwenye anga hapo jana.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice amesema atakuwa tayari kukutana na maafisa wa Iran endapo nchi hiyo itakomesha urutubishaji wa madini yake ya Uranium.

Mwandishi wa makala za uchunguzi nchini Marekani Seymour Hersh anadai kwamba Marekani inaweza kuanzisha mashambulio ya angani dhidi ya Iran katika kipindi cha saa 24 ikiwa rais Bush atatoa amri hiyo.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com