Teheran yajitayarisha kwa maandamano mengine | Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili | DW | 17.06.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Timu Yetu

Teheran yajitayarisha kwa maandamano mengine

Wafuasi wa mgombeaji aliyeshindwa nchini Iran, Mir Hossein Mousavi wamesema bado wataendelea na maandamano kwa siku ya nne, licha ya baraza kuu la sheria nchini humo kusema liko tayari kuhesabu baadhi ya kura.

Maandamano mjini Teheran

Maandamano mjini Teheran

Kwa siku nne mji wa Tehran ulileta zile kumbukumbu za yale mabadiliko ya Kiislamu ya mwaka wa 79. Maandamano ya kumuunga mkono rais Ahmedinejad na mengine yakupinga ushindi wake.

Wafuasi wa Mir Hossein Mousavi aliyeshindwa katika uchaguzi wa rais wamekuwa majiani wakidai kura zao ziliibwa na kumpa ushindi rais Ahmedinejad.

Kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei ambaye tayari alikuwa ameuunga mkono ushindi wa Ahmedinejad, amejirudi na kuliagiza baraza kuu la kisheria nchini Iran kuzihesabu tena baadhi ya kura kufuatia madai ya udanganyifu.

Baraza hilo la wanachama 12 wenye ushawishi mkuu na wenye uamuzi wa mwisho wa swala lolote lenye utesi Iran wamesema wako tayari kuzihesabu baadhi ya kura, na kutoa matokeo mapya chini ya siku kumi zijaazo. Lakini wametupilia mbali pendekezo la upinzani la kuyabatilisha matokeo ya uchaguzi. Ahmed Jannati ni mwenyekiti wa baraza hilo anasema lao ni jukumu la kisheria.

' ' Kulingana na sheria hatuna budi ila kukubali agizo la kiongozi mkuu Ayatollah na kuyachunguza upya matokeo ya uchaguzi, tuko tayari kutimiza jukumu letu ambalo ni la kisheria.'' Alisema Jannata.

Mousaavi na wafuasi wake hata hivyo wamelikataa pendekeo la baraza kuu la sheria wakisema dawa ya mzozo wa kisiasa Iran ni kufanyika kwa uchaguzi mpya. Na wamepanga kufanya maandamano mengine leo mjini Tehran.

Rais Ahmedinejad ambaye alirejea Iran leo, baada ya ziara ya siku moja mjini Moscow ameutetea tena ushindi wake akisema wingi wa kura alizopata ni dhahiri raia nchini Iran wana imani na uongozi wake. Jana viongozi wa China na Russia walimpongeza Ahmedinejad kwa ushindi wake.


Marekani hata hivyo bado inapima matamshi yake dhidi ya hali nchini Iran. Rais Barack Obama ambaye ameinyoshea mkonoi Iran baada ya miaka mingi ya kutofautiana kati ya Tehran na Washington, kuhusiana na mradi Iran wa Nyuklia, amesema hawezi kuingilia maambo ya ndani ya Iran lakini akaongeza ana wasiwasi kuhusiana na jinsi serikali inavyokabiliana na maandamano Iran.

'' Kutokana na uhusiano wa siku zilizopita kati ya Iran na Marekani si busara rais wa Marekani kuonekana anatia mkono wake katika uchahguzi wa Iran- lakini kama nilivyosema jana kunapotokea rabsha popote pale basi inakuwa ni kero kwangu na kwa wamarekani.'' Alisema Obama.

Jana wafuasi wa Ahmedinejad pia walifanya mkutano mkubwa pia nao kutoa sauti zao na kushtumu nchi za nje kwa kuingilia mambo ya ndani ya Iran.

Serikali ya Tehran pia imesema imewatia nguvuni baadhi ya viongozi wa upinzani wanaoidaiwa kushiriki na kupanga maandamano yaliyoibua machafuko nchini Iran. Usiku wa kumakia Jumatatu watu saba waliripotiwa kuuawa, baada ya siku nzima ya vurugu kati ya polisi wa kuzuia fujo na wafuasi wa Mousavi.

Mwandishi: Munira Muhammad/ RTRE

Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman


Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com