1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tatizo la Darfur bado ni swala nyeti.

Josephat Charo3 Septemba 2004

Huku umoja wa Afrika, AU, ukijiandaa kupeleka wanajeshi wake wa kulinda amani nchini Sudan, katibu mkuu wa umoja wa mataifa Dr Koffi Annan, anaomba misaada ya kifedha na vifaa vitakavyotumiwa na wanajeshi hao wanaokabiliwa na kibarua kigumu cha kumaliza mauaji yanayoendelea kwenye mkoa wa Darfur.

https://p.dw.com/p/CHia
Wanawake wa Darfur wakibeba kuni katika kambi ya Abu Shouk.
Wanawake wa Darfur wakibeba kuni katika kambi ya Abu Shouk.Picha: AP

Maafisa wa umoja wa mataifa wa ngazi za juu na wajumbe wa mashirika yanayoshughulikia misaada ya kiutu na mashirika yasiyo ya kiserikali, wana wasiwasi mkubwa kwamba nchi za Afrika hazina uwezo wa kiuchumi na wa kijeshi kiasi cha kuweza kugharamia shughuli za jeshi hilo. Hakuna uhakika kwamba mataifa ya magharibi yataingilia kati kusaidia hali ilivyo sasa.

Uongozi wa jeshi la Marekani katika Ulaya, USEUCOM, umeahidi kutoa ndege na vifaa vyengine vya kijeshi kusaidia harakati za umoja wa Afrika na usafiri wa wanajeshi katika eneo la Darfur. Madhumuni ya USEUCOM ni kuendeleza masilahi ya Marekani na Ulaya barani Ulaya, Afrika na Mashariki ya Kati.

Lakini mkurugenzi wa mipango ya kimataifa, Church World Service,CWS, mjini Washignton, Donna J Derr amesema hitaji muhimu ni fedha zitakazotumiwa kulipa mishahara ya wanajeshi.

Ikiwa kweli Marekani imesikia mwito uliotolewa na mashirika ya misaada ya kiutu na inataka kusaidia katika mpango huu wa kuleta amani huko Darfur, ni lazima itoe msaada wa kifedha mbali na vifaa.

Koffi Annan aliliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa mwezi uliopita kwamba Nigeria, Tanzania na Botwana zimeahidi kupeleka wanajeshi kushiriki katika jeshi la umoja wa Afrika. Afrika Kusini imekubali kutoa ushauri.

Mauaji ya Darfur ambako kadri waafrika elfu 30 wameuwawa na wengine zaidi ya milioni 1.5 kulazimika kuyahama makazi yao, yamefanywa na kundi la wanamgambo liitwalo janjaweed. Serikali ya Sudan inatuhumiwa kuunda kundi hili la magaidi na kufumbia macho mauaji yao ya safisha safisha.

Mjumbe maalumu wa umoja wa mataifa nchini Sudan Jan Pronk, ameliambia baraza la usalama la umoja wa mataifa kwamba Sudan inahitaji dola milioni 250 zaidi kama msaada wa kiutu hadi mwisho wa mwaka huu kusaidia wale walioyahama makazi yao kwa sababu ya ghasia za Darfur. Pronk ameilaumu jamii ya kimataifa kwa kupiga debe juu ya kusaidia wakimbizi wa Darfur.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa liliipa serikali ya Sudan siku 30 kukomesha mauaji yanayofanywa na wanamgambo wa janjaweed au iwekewe vikwazo vya kiuchumi na kijeshi.

Lakini bara hilo la mataifa 15, ambalo limekuwa likisita kuchukua hatua hiyo, sasa limeupa umoja wa Afrika jukumu hili, likiutaka kuongeza vikosi vya wanajeshi katika eneo la Darfur ambako tayari umoja huo una wanajeshi 300.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Africa Action mjini Washigton, Salih Booker, amesema shirika lake limeonya dhidi ya njama ya jamii ya kimataifa na baraza la usalama la umoja wa mataifa kuuwachia umoja wa Afrika jukumu la kukomesha mauaji ya halaiki huko Darfur. Umoja wa Afrika hauna uwezo wa kutatua tatizo la Darfur lakini unaweza kushiriki katika juhudi za kumaliza mzozo huo.

Kuna sababu tatu ambazo zinalifanya baraza la umoja wa mataifa kusita kuiwekea Sudan vikwazo. Kwanza kuna hofu kwamba jambo hilo huenda likatumika siku za usoni kama msingi wa kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyengine.

Pili, baadhi ya mataifa yanaamini sababu ya umoja wa mataifa kuingilia kati, ni kuiondoa Sudan kutoka uanachama na kuchukua mafuta yake na raslimali nyengine. Sababu ya tatu, hakuna fedha za kutosha za kugharamia na kuendeleza harakati hizo.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa lilishindwa kuchukua hatua za haraka kukomesha mauaji ya halaika ya mwaka wa 1994 nchini Ruanda ambako watutsi na wahutu elfu 800 waliuwawa.

Kuna tetesi kwamba mataifa yenye kura ya turufu katika baraza hilo zikiwemo Russia na Uchina, haziungi mkono kuwekewa vikwazo Sudan kwa sababu zina masilahi yake ya kibiashara na kiuchumi nchini humo. Kufikia sasa baraza hilo limegawanyika kuhusu swala hili.

Jan Pronk aliwaambia wajumbe kuwa hali ya Darfur bado ni mbaya. Ijapokuwa serikali ya Khartoum imefaulu kupeleka askari zaidi wa kulinda usalama na kuruhusu mashirika ya misaada ya kiutu kupeleka misaada katika eneo hilo, bado serikali ya Sudan imeshindwa katika sehemu mbili muhimu.

Sudan imeshindwa kuwadhibiti wanamgambo wa janjaweed na serikali haijachukua hatua zozote dhidi yao au kuwataja viongozi wao. Baraza la usalama la umoja wa mataifa litakutana juma lijalo kuamua hatua itakayochukuliwa.