1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yataka Kiswahili kitambuliwe lugha ya asili Afrika

Grace Kabogo
9 Februari 2021

Tanzania imeutaka Umoja wa Afrika kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya asili ya Afrika, na imesema kwamba hatua hiyo italeta msukumo mpya wa kuenzi juhudi za ukombozi katika eneo la kusini mwa Afrika.

https://p.dw.com/p/3p70P
Aussenminister Palamagamba Kabudi von Tansania
Picha: Getty Images/AFP/T.Karumba

Tanzania imewasilisha ombi hilo katika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kilichofanyika kwa njia ya mtandao na kuongozwa na mwenyekiti anayemaliza muda wake, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa. Serikali ya Tanzania imejaribu kubainisha sababu ya kutaka lugha hiyo inayozungumzwa karibu katika eneo lote la Afrika Mashairki na Kati na maeneo mengine ya mbali, irasimimishwe kuwa lugha ya asili katika bara hili lenye nchi 53.

Kiswahili tunu ya Afrika

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi aliyeshiriki kikao hicho kwa niaba ya Rais John Magufuli amesema Kiswahili ni tunu ya Afrika na zaidi ya yote ni lugha inayobeba alama ya ukombozi katika eneo lote la kusini mwa Afrika, hivyo kuifanya kuwa lugha ya asili itakuwa ni jambo jema.

Kumbukumbu za ukombozi katika eneo la kusini mwa Afrika zinaoonyesha kwamba, wapigania uhuru katika eneo hili walipiga kambi nchini Tanzania wakiendesha harakati za utawala wa kikoloni na wakati wote huo walilazimika kujifunza na kuitumia lugha hiyo kufikia malengo yao.

Südafrika Präsident Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika aliyemaliza muda wakePicha: Getty Images/AFP/P. Magakoe

Hivi karibuni lugha ya Kiswahili ilianza kutumika rasmi katika vikao vya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, ikiwa miaka kadhaa imepita tangu Umoja wa Afrika ukifanye Kiswahili kama lugha inayotumika katika vikao vyake.

Mbali ya kutaka lugha hii kutambulika kama lugha ya asili ya Afrika, serikali ya Tanzania imeongeza shabaha nyingine ikitaka pia, maeneo yaliyotumiwa na wapigania ukombozi kusini mwa Afrika kuenziwa na kutambulika kama ni moja ya maeneo ya urithi wa kimataifa.

Msukumo wa Kiswahili

Katika miaka ya hivi karibuni lugha hii imekuwa ikipewa msukumo mpya wa kutaka ipate umaarufu mkubwa katika eneo la kusini mwa Afrika, ikiwamo juhudi za kutaka ifundishwe kuanzia shule za awali mpaka vyuo vikuu.

Hata hivyo, hatua ya kutaka kuifanya iwe lugha ya asili ya Afrika huenda ikaibua mjadala mkubwa hasa kwa wale wanaiona kuwa lugha hii imetokana na mkusanyiko wa maneno kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Wengi wa hao wanasema kwamba, lugha ya Kiswahili haibebi uhalisia wa moja kwa moja wa lugha ya Kibantu wakisema sehemu kubwa ya maneno yake yametoholewa kutoka lugha nyingine kama Kireno, Kijerumani na Kiarabu kwa sehemu kubwa. Ingawa baadhi ya wafuatiliaji wanasema Kiswahili bado kinaendelea kuakisi uasili wa Kiafrika na ni lugha yenye asili kubwa ya kibantu.