1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yakabidhi uenyekiti wa SADC kwa Msumbiji

Grace Kabogo
17 Agosti 2020

Tanzania imekabidhi uwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SDC kwa Msumbiji huku jumuiya hiyo ikifikisha miaka 40 tangu kuasisiwa kwake.

https://p.dw.com/p/3h5Ox
Afrika Tansania Mosambik SADC  John Magufuli
Picha: DW/D. Khamis

Wakati akikabidhi uenyekiti huo, Rais John Magufuli ameonyesha wasiwasi wake kuhusu kasi ndogo ya ufanyaji biashara miongoni mwa nchi wanachama hali ambayo amesema inarudisha nyuma shabaha ya ukuzaji uchumi.

Jumuiya hiyo ambayo ilianza na nchi tisa na hatimaye kufikisha 16 bado inatajwa kujikongoja kufungua milango ya kufanya biashara miongoni mwa nchi wanachama kunakochangiwa na sababu mbalimbali kama vile vikwazo na mlolongo wa sheria zisizo rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara.

Nchi za SADC zinapaswa kushirikiana

Kwa kutambua hilo, Rais Magufuli aliyekabidhi uenyekiti wa jumuiya hiyo kwa Rais wa Msumbiji, Felipe Nyusi amesema nchi za SADC zinapaswa kuamka.

Mkutano huo wa kilele ulioendeshwa kwa njia ya mtandao kutokana na janga la virusi vya corona, umekuwa jukwaa pia la kutaja mafanikio ya kipindi cha mwaka mmoja tangu Tanzania ilipokabidhiwa uenyekiti wa mzunguko.

Utatuaji wa mizozo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Lesotho, uimarishaji wa amani na ulinzi ndani ya jumuiya hiyo pamoja na kuendeleza ushirikiano wa kisiasa ni baadhi ya mambo yaliyozingatiwa ndani ya mwaka huo mmoja.

Afrika Tansania Mosambik SADC  John Magufuli
Rais wa Tanzania, John MagufuliPicha: DW/D. Khamis

Hata hivyo, ingawa wakati fulani Tanzania ilitupiwa lawama kutokana na kujitenga na mataifa mengine katika kulishughulikia janga la virusi vya corona, Rais Magufuli amesema nchi za SADC zimeendelea kufanya kazi kwa pamoja katika kulishinda janga hilo.

Ametoa wito kwa mataifa yaliyoendelea kuweka mpango maalumu kwa kuyasamehe madeni mataifa ya dunia ya tatu ili yajikwamue na janga hilo.

Jumuiya hiyo ya SADC iliyoasisiwa miaka 40 iliyopita na waliokuwa wapigania uhuru wa nchi za Kusini mwa Afrika, hivi sasa inakadiriwa kuwa na idadi ya watu wanaofikia milioni 350, kutoka watu milioni 60 wakati ilipoanzishwa. Pamoja na kuendelea kuwa na ajenda ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, pia jumuiya hiyo imekuwa ni jukwaa muhimu la utanzuaji wa mizozo kwa nchi wanachama ikiwamo ile inayohusiana na masuala ya uchaguzi.