Tanzania yafanya uchaguzi kukiwa na hofu ya kutokea ghasia | Matukio ya Afrika | DW | 28.10.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tanzania yafanya uchaguzi kukiwa na hofu ya kutokea ghasia

Mamilioni ya Watanzania wanapiga kura katika uchaguzi ambao wapinzani tayari wanalalamikia visa vya kunyanyaswa, Rais John Magufuli anayewania muhula wa pili, amesema kutunza amani ni suala lenye kipaumbele.

Wakati misururu mirefu ya wapigakura ikishuhudiwa katika vituo vya uchaguzi nchini Tanzania, mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe amearifu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa tweeter, kwamba maisha yake yako hatarini. Amesema ''genge la watu waliojihami kwa silaha'' huku wakilindwa na polisi wameivamia hoteli yake na kuwakamata walinzi wake wawili.

Hapo jana pia kuliripotiwa vurugu kubwa visiwani Zanzibar, ambako chama kikuu cha upinzani upande huo cha ACT Wazalendo, kiliituhumu polisi kuwauwa wafuasi wake tisa.

CHADEMA pia iliwashutumu wafuasi wa chama tawala, CCM kuwauwa watu wawili kwa bunduki katika mkutano wa CHADEMA uliofanyika katika mji ulio kaskazini-mashariki mwa Tanzania.

Shirika la habari la Associated lililoripoti ya visa hivi, limesema juhudi zake za kutaka maelezo kutoka CCM hazikupata majibu.

Hisia mseto miongoni mwa wapigakura

Tazama vidio 01:54

Je wewe tayari umekwishapiga kura?

Mpigakura wa visiwani Zanzibar, Yahya Khamis aliyezungumza na shirika hilo, alisema haamini kama uchaguzi huu utakuwa huru wala wa haki. Khamis amesema wakati akitakiwa kupiga kura kwa wagombea watano, amepigwa na mshangao alipokabidhiwa karatasi nne za kupigia kura.

Hata hivyo, mpiga kura mwingine kutoka huko huko Zanzibar, Jokha Mohammed, amesema anajisikia kuwa na uhakika wa usalama wake, kutokana na maafisa wengi wa jeshi na polisi wanaopiga doria mitaani.

Baada ya kupiga kura yake asubuhi ya leo mjini Dodoma, rais wa Tanzania anayewania muhula wa pili John Pombe Magufuli, amesema ''kuhifadhi amani ni suala lenye kipaumbele''. Magufuli ameunga mkono demokrasia, na kuwataka Watanzania wote kwenda kupiga kura zao.

Magufuli ashutumiwa kutawala kwa mkono wa chuma

Rais Magufuli anayejinadi kama mtetezi wa wanyonge, amejijengea jina kwa kupambana na rushwa, lakini mashirika ya kimataifa ya kutetea haki ya binadamu yanamshutumu kuvikaba koo vyombo vya habari na kuminya uhuru wa mashirika ya kiraia, huku pia akiukandamiza upinzani wa kisiasa.

Tangu mkesha wa tarehe ya uchaguzi, mtandao wa intaneti umepunguzwa nguvu, na kutatiza mawasiliano ya watu katika mitandao ya kijamii.

Ni waangalizi wachache tu walioruhusiwa kwenda kutazama namna zoezi hili la uchaguzi linavyoendelea, na vyama vya upinzani vimelalamika, vikisema maelfu ya mawakala wao wamenyimwa vibali vya kuwa waangalizi. 

Kwa upande wa vyombo vya habari vya kimataifa, ni vichache tu vilivyopata ruhusa ya kupeleka waandishi katika maeneo ya uchaguzi.

Alama ya kuuliza juu ya sifa ya Tanzania kama kisiwa cha amani

Wanadiplomasia na taasisi za kimataifa pia wamekuwa wakielezea wasiwasi kwamba Tanzania iliyojulikana kama kisiwa cha amani na mpatanishi wa kikanda, yenyewe taratibu inajikuta katika mgogoro lihusikapo suala la haki za binadamu.

Mshindani mkuu wa Rais Magufuli katika uchaguzi huu, Tundu Lissu anayegombea urais kwa tiketi ya CHADEMA alinusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa risasi mwaka 2017, na amerejea nchi mwake mwaka huu baada ya kupata matibabu ya muda mrefu ughaibuni.

Katika kipindi hiki cha kampeni alitumikia adhabu ya kutofanya kampeni kwa siku saba, baada ya kushutumiwa na mamlaka kutamka maneno ya uchochezi.

Kundi la uangalizi linalowajumuisha watu maarufu kutoka ukanda wa Afrika Mashariki, limezungumzia kuwepo kwa hotuba za vitisho, na kuonya kuwa ikiwa kura ingepigwa katika mazingira kama hayo, uchaguzi ungekuwa na kasoro.

Vyanzo: ape, afpe