1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania na demokrasia kuelekea kwenye uchaguzi mkuu

Grace Kabogo
15 Septemba 2020

Leo ni Siku ya Kimataifa ya Demokrasia na huko nchini Tanzania siku hii inaadhimishwa wakati taifa hilo likielekea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.

https://p.dw.com/p/3iUGw
Tansania Dodoma Veröffentlichung Parteiprogramm der CCM
Picha: DW/E. Boniphace

Kumekuwa na maoni mengi yanayotofautiana kuhusiana na dhana ya demokrasia ya kweli katika taifa hilo la Afrika Mashariki ambalo linatajwa kuwa kitovu cha amani katika ukanda huo.

Demokrasia kama inavyoelezwa na wengi ndiyo msingi wa mambo yote katika mustakabali wa taifa na kuadhimishwa kwake tarehe 15.09 kunatiliwa maanani zaidi nchini Tanzania hasa wakati ambako vyama vya siasa pamoja na wafuasi wao wanaendelea kupishana katika majukwaa ya kampeni kunadi sera zao.

Kwa ujumla inaweza kuelezwa kwamba Tanzania ni miongoni mwa mataifa yanayoenzi demokrasia na mara zote watendaji walioko katika mamlaka wamekuwa wakitumia mifano kama utitiri wa vyombo vya habari pamoja kuwepo kwa idadi kubwa ya wagombea wanaojitokeza kwenye uchaguzi ni moja ya vielelezo kuthibitisha hoja hiyo.

Hata hivyo, bado kuna ukosoaji mkubwa unaendelea kutanda hasa kunapozuka mjadala kwamba ni kwa kiasi gani taifa hilo liko katika mkondo sahihi kuhusu demokrasia ya kweli. Baadhi wanaojadili mambo hayo wanasema Tanzania kama ilivyo mataifa mengine duniani, bado ina safari ndefu kufikia kile kinachoitwa demokrasia inayotoa fursa ya kuwaridhisha walio wengi.

Tansania Wahlkampagne Tundu Lissu, Kandidat der Opposition
Mgombea wa urais kupitia chama cha Chadema, Tundu LissuPicha: Getty Images/AFP

Mchambuzi wa masuala ya siasa na utawala, Sammy Ruhuza ni mmoja wa wale wanaoona kwamba Tanzania bado inaendelea kuvuta miguu kifikia shabaha ya demokrasia yenye kutoa usawa kwa washiriki wote wa masuala ya siasa na uchaguzi.

Uchaguzi wa mwaka huu unatoa ishara kwamba uwanja wa demokrasia kwa watu kuchagua na kuchaguliwa umetanuka. Jumla ya wagombea 15 wamepitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC kuwania urais, ingawa kumekuwa na malalamiko mengi namna wagombea wa upinzani wa nafasi ya ubunge na udiwani walivyoenguliwa katika hatua za awali.

Ikiwa ni uchaguzi wa sita kufanyika tangu Tanzania irejeshe mfumo wa vyama vingi mmano mwaka 1992, kuna matumaini pia uchaguzi wa mwaka huu ukavuka salama. Hungwi Maliatabu na mwalimu wa masomo ya uraia anasema, wakati duniani inapoadhimisha siku ya demokrasia, raia wanayo haki ya kipekee katika uchaguzi huu.

Jumla wa wapiga kura milioni 29 wameandikishwa kushiriki uchaguzi huu ni wengi wao sasa wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kufuatilia mikutano ya wagombea kabla ya kufanya maamuzi yao Oktoba 28, 2020. Wagombea wote wa urais wanaendelea kuyazunguka maeneo ya nchi wakianisha vipaumbele ambavyo wanaahidi kuvizingatia iwapo watachaguliwa.