Tanzania: Waandishi wa habari wa CPJ wakamatwa na kuachiwa | Matukio ya Afrika | DW | 08.11.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tanzania: Waandishi wa habari wa CPJ wakamatwa na kuachiwa

Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini imesema wafanyakazi wawili wa Shirika Linalotetea Haki za Waandishi, CPJ waliokuwa wamekamatwa nchini Tanzania, wameachiwa huru, lakini bila kurejeshewa hati zao za kusafiria.

Logo CPJ (APTN)

Kulikuwepo hali ya sintohamu baada ya taarifa kwamba maafisa hao, Angela Quintal ambaye ni raia wa Afrika Kusini na Muthoki Mumo kutoka Kenya, walikuwa wamezuiliwa katika chumba chao cha hotel mjini Dar es Salaam na watu waliojitambulisha kama maafisa wa uhamiaji, bila kupewa maelezo yoyote.

Shirika linalotetea haki za waandishi wa Habari CPJ limesema Bi Quintal ambaye ni afisa wake anayeshughulikia masuala ya uhuru wa vyombo vya habari barani Afrika na mwenzake Mumo, kuwepo kwao nchini Tanzania hakukukiuka sheria yoyote. CPJ ilisema maafisa waliowazuilia hotelini walipekuwa mizigo ya Quintal na Mumo, na kuzichukuwa hati zao za kusafiria, na kisha wakawatoa hotelini kwao na kuwapeleka mahali pasipojulikana.

Utata kuhusu akaunti za twitter

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo, ujumbe wa kutiliwa mashaka ulitumwa kutoka akaunti ya twitter ya Angela Quintal, ukisema ''Mungu ni mkubwa, tumeachiwa na tunarudi hotelini.'' Baadaye, akaunti za mitandao ya kijamii za wafanyakazi hao zilikuwa zimefungwa.

Asubuhi ya leo wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini, kupitia msemaji wake imearifu kuwa wafanyakazi hao wa CPJ walikuwa wameachiwa huru, na kwamba wote wawili walikuwa katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Dar es Salaam. Msemaji wa wizara hiyo, Ndhivo Mabaya ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kuachiwa kwao kuliwezekana baada ya miito mingi kutolewa, na kwamba walikuwa wakijaribu kufahamu undani wa sababu za kukamatwa kwao.

Baadaye wizara hiyo iliarifu kupitia ukurasa wake wa twitter, kwamba Quintal na Mumo walikuwa wakifanya mazungumzo na balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania.

Tanzania yachunguza kujua wahusika

Kwa upande wa serikali ya Tanzania, msemaji wa Idara ya Uhamiaji Ali Mtanda ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba walikuwa wakifuatilia kwa karibu kukamatwa kwa wafanyakazi hao wa CPJ, wakitaka kujua kwa uhakika taasisi ya serikali iliyohusika.

Tangu kuingia madarakani kwa rais John Pombe Magufuli miaka mitatu iliyopita, utawala wake unashutumiwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari na kuyafungia baadhi ya magazeti yanayoikosoa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe, rtre

Mhariri: Mohammed Khelef