1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Kukithiri kwa dawa za kuongeza nguvu za kiume

Bruce Amani
29 Aprili 2019

Kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu za kiume kwa baadhi ya wanaume, hatimaye suala hilo limetua bungeni nchini Tanzania.

https://p.dw.com/p/3HcXQ
Viagra
Picha: picture-alliance/dpa/U.Deck

Baadhi ya wabunge wamehoji ni hatua gani zimechukuliwa na serikali ili kubaini ni nini kinachosababisha kuwepo na tatizo hilo ambalo limesababisha kuwepo utitiri wa dawa za kuongeza nguvu za kiume zinazouzwa mtaani huku zingine zikiwa hazijathibitishwa na mamlaka ya chakula na dawa nchini humo, TFDA.

Suala hilo la tatizo la upungufu wa nguvu za kiume kwa baadhi ya wanaume nchini Tanzania limeibuka bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali na majibu ambapo mbunge Goodluck Mlinga kupitia CCM aliihoji serikali endapo kama imekwishafanya utafiti ni nini kinachosabisha kuwepo kwa tatizo hilo hadi kuwafanya baadhi ya wanaume kukimbilia kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo kwa hivi sasa zimekuwa zikiuzwa katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Hussein Mwinyi
Waziri wa Ulinzi nchini Tanzania Hussein MwinyiPicha: gemeinfrei

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Hussen Mwinyi amesema tatizo la upungufu wa nguvu za kiume linasababishwa na magonjwa mbalimbali ikiwemo kisukari na msongo wa mawazo na kwa hivi sasa linaonekana kuwa kubwa na hata kusababisha baadhi ya wanaume kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo na kuongeza kuwa:

Katika hatua nyingine serikali ya Tanzania imesema haitazifungia saloon za kike zinazojishughulisha na masuala ya urembo wa kina mama ikiwemo uwekaji kucha na kope za bandia kwa kile ilichosema kuwa haijawahi kupokea taarifa za madhara kuhusiana na kucha pamoja na kope za kubandika na kwamba kutokana na kukosekana na takwimu zozote zinazoonyesha madhara kamwe haiwezi kuchukua hatua yoyote dhidi ya watoa huduma hizo.

Awali katika kipindi cha maswali na majibu hii leo bungeni, mbunge Rukia Kassim Ahmed wa viti maalum CCM alisema kuwa kuna baadhi ya wanawake wameathirika na matumizi ya dawa za kuongezea makalio pamoja na matumizi ya kope na kucha bandia, kauli ambayo imepokelewa kwa hisia tofauti na wamiliki na watoa huduma za urembo katika saloon mbalimbali mjini Dodoma.

Katika mkutano uliopita wa kumi na Nne wa bunge la Tanzania, Spika wa bunge Job Ndugai alipiga marufuku wabunge na wageni wote wenye na kucha na kope bandia kutoingia bungeni.