1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania: Kufunga shule Longido kufuatia uvamizi wa nzige

Amina Mjahid
22 Februari 2021

Serikali ya Tanzania imetangaza kuzifunga kwa muda baadhi ya shule zilizopo katika wilaya ya Longido, eneo linalopakana na kaunti ya Kajiado nchini Kenya ili kutoa nafasi ya kukabiliana na nzige katika wilaya hiyo.

https://p.dw.com/p/3pgq0
Afrika Heuschreckenplage in Kenia
Picha: Tony Karumba/AFP/Getty Images

Nzige hao ambao wanaelezwa kutokea nchini Kenya tayari wameonekana kusambaa katika wilaya za Longido na Simanjiro zilizopo katika mikoa ya kaskazini mwa Tanzania.

Makundi makubwa ya Nzige yalishuhudiwa katika wilaya ya Longido  mkoa wa Arusha Tanzania kuanzia siku ya ijumaa wiki iliyopita, na kuzua taharuki kwa baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo ambao wengi wao ni wafugaji.

soma zaidi:Watafiti Kenya watafuta njia ya kuwaangamiza nzige

Mkuu wa wilaya ya Longido Frank Mwaibambe amesema kuwa watakabiliana na makundi hayo ya Nzige kwa kunyunyiza dawa kwa kutumia ndege ya shirika la chakula duniani FAO inayotokea Nairobi nchini Kenya zoezi linalotarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Longido Juma Mhina ametoa maagizo ya kufungwa kwa shule zote ambazo zitapitiwa na oparesheni hiyo ya kukabiliana na Nzige.

Hakuna madhara yoyote hadi sasa yaliosababishwa na uvamizi wa Nzige

Kenia Meru | Heuschreckenplage & Landwirtschaft
Picha: Yasuyyoshi Chiba/AFP/Getty Images

Mamlaka za serikali  zinasema mpaka sasa hakuna madhara yeyote yaliyojitokeza.

Mamlaka hizo zimesema eneo lililovamiwa na Nzige hao kwa kiasi kikubwa ni pori na Nzige waliovamia bado ni wadogo.

Waziri wa kilimo Profesa Adolf Mkenda anasema mbali na wilaya ya Longido, pia oparesheni hiyo itafanywa katika wilaya ya Simanjiro iliyopo mkoani Manyara ambapo makundi hayo ya Nzige pia yameonekeana.

Mwaka uliopita wa 2020, makundi makubwa ya Nzige yalivamia maeno kadhaa ya nchi za Kenya na Ethiopia na kuibua hofu ya kutokea kwa baa la njaa kutokana uharibifu mkubwa wa mazao.

Mpaka tunakwenda mitamboni, baadhi ya maofisa wa serikali wanaohusika wapo wilayani Longido wakisubiri ndege kutoka Nairobi na wakiainisha maeneo ambayo yatanyunyiziwa dawa.

Lakini kuna habari zinazoeleza kwamba makundi hayo ya Nzige kwa sasa hayaonekani.

Mwandishi: Veronica Natalis DW