1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania kuchangia kupambana na ugaidi nchini Msumbiji

George Njogopa25 Machi 2022

Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kuimarisha nguvu ya pamoja kwa lengo la kukabiliana na vikundi vya kigaidi vinavyoendeleza mashambulizi nchini Msumbiji.

https://p.dw.com/p/4923j
Präsident von Mosambik besucht Militärstützpunkt
Picha: Roberto Paquete/DW

Hayo yamefikiwa kwa pamoja katika kikao kilichowakutanisha wakuu wa nchi hizo, kilichomalizika nchini Jordan ambacho kiliitishwa na Mfalme Abdullah II , ambaye ni mwenyekiti wa nchi zinazojishughulisha na mapambano dhidi ya ugaidi.

Mkutano huo ni wa tatu kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 na huwakutanisha viongozi wakuu wa nchi za ukanda wa Mashariki ya Afrika kwa lengo la kujadili changamoto za ugaidi na namna ya kuudhibiti.

Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majliwa amesema Tanzania haitaitupa mkono Msumbiji katika kukabiliana na ugaidi, kwa vile vitendo hivyo vinafanyika katia eneo ambalo ni karibu na mpaka wa Tanzania.

''Tayari mjadala na maamuzi yametolewa namna nzuri ya kushiriki katika mapambano dhidi ya ugaidi.''

Kwa miaka kadhaa sasa Msumbiji imekuwa ikiandamwa na mfululizo wa mashambulizi yanayodaiwa kufanywa na wapiganaji wa msituni wenye mafungamano ya Dola ya Kiislam(IS) kundi ambalo pia limekuwa likiendesha mapigano katika maeneo mengine duniani.

Soma pia→SADC yazindua kituo cha kupambana na ugaidi

''Tutaendelea kusaidia Msumbiji kwa kiwango wanachokihitaji''

Tansania Premier Minister Kassim Majaliwa
Picha: DW/V. Natalis

Kumekuwa na juhudi za pamoja kutoka nchi wanachama wa jumuiya ya maendeleo kusini mwa Afrika(Sadc) kuwadhibiti wapiganaji hao wanaoendesha uasi katika mkoa wa Cabo Delgado, huku wakiwatesa na kuwaua raia.

Kikao hicho cha Jordan  ambacho pia kimehudhuria na Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi pamoja na marais wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kimeahidi kuzidisha mbinyo kwa wapiganaji hao ambao pia wamewahi kuuteka mji wa Palma ulioko karibu maili sita kutoka mradi mkubwa wa gesi asilia katika bahari ya Hindi karibu na mpaka wa Msumbiji na Tanzania.

''Tunaeleza namna ambayo tunaweza kumsaidia Msumbiji,lakini tunawahakikishia pia Umoja wa Mataifa kwamba Tanzania iko mustari wa mbele pia katika hili la kupambana na magaidi, na tutaendelea kusaidi Msumbiji kwa kiwango wanachokihitaji.''

Soma pia→Rwanda yakiri kupoteza askari wanne huko Cabo Delgado

Tangu 2017, wapiganaji hao wamefanya mamia ya uvamizi, wakisababisha vifo kwa idadi ya watu isiyojulikana huku zaidi ya watu 700,000 kukimbia makazi yao ili kunusuru maisha.Hadi sasa hajafahamika wazi nini kiini cha kuanzisha mashambulizi hayo yanayoliweka katika hali tete eneo la kaskazini mwa Msumbiji.