Tanzania kubana usajili wa meli za mizigo | Matukio ya Afrika | DW | 18.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tanzania kubana usajili wa meli za mizigo

Serikali ya Tanzania imeunda kikosi kitakachochunguza usajili wa meli za kimataifa, baada ya kukamatwa kwa meli mbili zilizokuwa zikipeperusha bendera ya taifa hilo zilizodaiwa kusafirisaa silaha na madawa ng'ambo.

Makamu wa Rais Samia Suluhu amesetangaza hatua hiyo wakati alipokutana na waandishi wa habari Ikulu mapema Alhamisi, kuzungumzia sakata la kunaswa kwa meli mbili ambazo zinadaiwa kukiuka mikataba ya kimataifa kwa kusafirisha makontena ya silaha na dawa za kulevya.

Moja ya meli hizo ilinaswa katika bahari ya Jamhuri ya Dominica ikiwa na shehena ya dawa za kulevya na nyingine ikakamatwa huko Uturuki ikisafirisha silaha zilizodaiwa kupelekwa Misri lakini  baadaye ikabainika ilikuwa safarini kwenda Libya.

Katika mkutano wake huo na waandishi wa habari, Makamu wa Rais Samia mbali ya kulaani kitendo hicho alisema pia kwamba Tanzania sasa inachukua hatua mpya katika usajili wa meli zote ikiwamo za nyumbani na zile za kimataifa ili kudhibiti tabia ya aina hiyo.

Hadi Disemba mwaka jana, Tanzania ilikuwa imesajili meli za nje zinazofikia 457 zikiwemo zile kutoka Marekani, Uturuki na maeneo ya Asia wakati meli za ndani zilizosajiliwa zilikuwa 64. Meli hizo hufanya safari maeneo mbalimbali duniani zikiwa na bendera ya Tanzania.

Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira Januari Makamba amekiri changamoto inayoikabili Tanzania katika kukabiliana na uhalifu wa namna hiyo lakini akaahidi kushirikiana na kikosi kipya kilichoundwa kushughulikia kadhia hiyo.

Meli hizo bado zinaendelea kuchunguzwa katika mataifa zilikokamatwa na Tanzania imewataka wamiliki wake kushusha mara moja bendera yake. Kumekuwa na matukio ya mara kwa mara kwa meli za kimataifa kumamatwa zikikiuka makubaliano ya kimataifa huku zikipeperusha bendera ya Tanzania.

Mwandishi: George Njogopa

Mhariri: Daniel Gakuba