Tanzania: Kabendera amwomba radhi Rais Magufuli | Matukio ya Afrika | DW | 01.10.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Tanzania: Kabendera amwomba radhi Rais Magufuli

Mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Eric Kabendera aliye rumande akikabiliwa na tuhuma za kuhujumu uchumi amemwomba radhi Rais John Magufuli, iwapo alimkosea katika kutekeleza majukumu yake ya kiuandishi

Kabendera anayekabiliwa na mashtaka matatu ikiwamo lile la utakatishaji fedha ametoa ujumbe huo kupitia wakili wake aliyesema kwa niaba ya familia na wanataalumu wanzake, angependa kumwomba radhi Rais John Magufuli.

Mmoja wa mawikili hao, Jebra Kambole amesema kwa niaba ya mteja wao angependa kufikisha ujumbe huo kwa Rais na kwamba kama kuna kosa lolote alilolifanya wakati akiwa kwenye majukumu yake ya uandishi basi anaomba radhi.

Kabendera ambaye alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Agosti 5 na kusomewa mashtaka matatu ya ubadhirifu wa uchumi, kesi yake itasikilizwa tena Oktoba 11 wakati waendesha mashtaka wakiendelea na upelelezi.

Mawakili wake, mbali ya kutoa ujumbe wa kuombna radhi, wameomba pia kuharakishwa upelelezi wa mashtaka yanayomkabili mteja wao ambaye anaripotiwa pia kukabiliwa na tatizo la mguu.

Anatuhumiwa kwa makosa yapi?

Mwandishi huyo aliyekuwa akifanya kazi na mashirika ya ndani na yale ya nje ya nchi anatuhumiwa kujihusisha na genge la uhalifu, huku shitaka jingine likiwa ni la ukwepaji wa kodi zaidi ya milioni 170. Kadhalika anakabiliwa na shtaka la tatu la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni 170.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyafanya hayo kati ya Januari 2015 na Julai mwaka huu mjini Dar es Salaam na kwa baadhi ya makosa anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano wa watu ambao hawakuwepo mahakamani.

Tansania Erick Kabendera vor Gericht (DW/S. Khamis)

Erick Kabendera akiwa na mmoja wa mawakili wake kwenye mahakama ya Kisutu Agosti 5 mwaka huu

Makosa yote hayana dhamana na Kabendera anaendelea kusota rumande tangu alipokamatwa kwa mara ya kwanza Julai 29 akiwa nyumbani kwake maeneo ya Mbweni. Wakati hayo yakiendelea, Rais John Magufuli ambaye amekuwa akijipambanua kama kiongozi aliyevalia njuga masuala ya rushwa na ufisadi ameongeza muda wa siku saba kwa watuhumiwa walioko rumande wanaokabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ambao wako tayari kukiri na kulipa kiasi cha fedha kitakachokubaliwa na mwendesha mashtaka wa serikali.

Hadi jana wale waliojitokeza kuandika barua kwa mwendesha mashtaka wakikiri makosa hayo ilifikia watuhumiwa 467 na ripoti zinasema huenda idadi hiyo ikaongezeka katika kipindi hiki cha siku saba zilizoongezwa.

 

DW inapendekeza