1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania inavyopambana na njaa iliojificha

22 Juni 2018

Wataalamu wa masuala ya lishe wanaeleza njaa iliojificha kuwa ni kula chakula na kushiba huku mwili ukiwa haujavuna vya kutosha madini, protini na hata vitamin, hali inayopelekea mwili kuzongwa na maradhi mbalimbali.

https://p.dw.com/p/306oP
Proteinquellen
Picha: Colourbox

Mataifa yanayoendelea yamekuwa yakikabiliwa kwa kiasi kikubwa na matatizo ya lishe kutokana na wananchi wengi kutokuwa na elimu ya kutosha na sahihi juu ya lishe bora katika familia zao, hali inayoathiri kasi ya juhudi za kupambana na njaa iliojificha.

Tanzania  ni miongoni mwa mataifa yanayokabiliwa na tatizo hilo kwa watu wake hasa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wanawake walio katika rika la kuzaa.

 Utafiti wa wa afya na viashiria vya malaria wa mwaka 2015/16 unaonesha kuwa upungufu wa damu kwa watoto walio na umri wa miezi 6 hadi 59 ni asilimia 58 huku asilimia 2 wakiwa na upungufu wa juu wa damu, asilimia 30 wakiwa na upungufu wa kati na asilimia 26 wakikabiliwa na upungufu wa damu wa kawaida.

Utafiti huo unaonyesha kuwa mkoa wa Shinyanga ndiyo umeathirika zaidi ambapo wastani wa asilimia 71 ya watoto wana tatizo la upungufu wa damu.

Bado utafiti huo unaonyesha kuwa miongoni mwa wanawake walio katika rika la kuzaa la umri wa kuanzia miaka 15-49 asilimia 45 wana tatizo la upungufu wa damu ambapo asilimia 1 wana upungufu wa damu wa juu, asilimia 11 wana upungufu wa damu wa kati na asilimia 33 wakiwa na upungufu wa damu kawaida.

Tansania Jackfruits-Verkäufer in Dar es Salaam
Fenesi ni tunda lenye manufaa makubwa katika mwili wa mwanadamu.Picha: DW/S. Khamis

Udumavu na utapiamlo kwa dhana ya kitabibu

Wataalamu wa masuala ya lishe waliiambia DW kuwa udumavu ni matokeo ya  utapiamlo mkali unaotokana na mtoto kukosa lishe bora katika kipindi cha siku elfu moja tangu kutungwa kwa mimba.

Hivyo mtu huwa na uzito usioendana na umri wake, katika makala hii Ruthy Mkopi, afisa mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe nchini Tanzania (TFNC) anasema mapambano dhidi ya udumavu laazima yaanze katika siku 1000 za kwanza za binadamu.

"Hizi tunazihesabu tangu kutungwa kwa mimba ambapo hapa mama anatakiwa ale chakula kwa uwiano sawa katika kila kundi la  chakula, kwa maana ya mikunde, asili ya wanyama, mbogamboga, sukari, mafuta pamoja na matunda", alisema mkopi na kuongeza kuwa, "akila kwa mgawanyiko sahihi itasaidia kwa kiwango kikubwa kupata mtoto ambae hajadumaa."

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema utapiamlo ambao matokeo yake ni udumavu hutokana na kutokuwa na usawa katika kiwango cha chakula kinachompa mtu virutubisho mwilini.

Hali hii hutokea kwenye makundi mawili; kwanza kutokuwa na lishe ya kutosha ambako kunajumuisha kudumaa, kuwa  na uzito mdogo usioendana na umri pamoja na kukosa virutubisho vya kutosha.

Pili ni kula vyakula vinavyoleta  unene uliopitiliza na magonjwa yanayotokana na mtindo wa maisha. Na hali hii huwapata zaidi watoto na watu wenye kipato kizuri waishio mjini.

Mkopi anasema "kaya nyingi hasa za mjini zina utamaduni wa kula vyakula vya jamii ya wanga ambavyo ni kama  ugali wa mtama, mahindi, na muhogo na wali, huku akibadilisha mboga peke yake lakini anakuwa amekula chakula cha jamii ya aina moja pekee yake kwa siku nzima”

Simbabwe Kartoffelverkäuferin in Harare UN FAO Hunger und Biosprit
Mwanamke akiuza viazi.Picha: AP

 Hali ilivyo ndani ya kaya

Katika familia nyingi linalotazamwa ni kula na kila mwanafamilia ashibe kwa kiwango chake pamoja na urahisi wa upatikanaji wa chakula katika jamii husika, ndani ya familia nyingi wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto walio chini ya miaka mitano ndio wanaathirika zaidi na tatizo hili linalotajwa na wataalamu njaa ilio jificha.

Mkazi wa jijini dar  es salaam Siwema Shukuru (33) amezaa watoto wawili na walikumbwa na tatizo la udumavu. Anasema haamini suala la chakula kama linaweza kusababisha mtoto wake mwenye miezi 22, anaeanza kutambaa ashindwe kukua kama watoto wengine walio katika umri wake ambao kwa kawaida wameanza kuzungumza, kukimbia huku na kule kwa kujifunza na hata utundu wenye kugundua zaidi.

"Ni mtoto wangu wa pili wa kwanza alifariki kwa tatizo la upungufu wa damu, sitaki kuamini kama chakula kinasababisha, sababu asubuhi nampa uji wa mahindi ikifika mchana tunakula ugali usiku kwenye saa nne tunakula kama ni wali ama ugali, yeye nilimuachisha kunyonya tangu alipotimiza mwaka mmoja,” anasema siwema.

Hali ya siwema inatajwa na wataalamu kuwaathiri zaidi wanawake walio vijijini ambao wao kwa kiasi kikubwa ndio wanatazamwa kama wazalisaji ndani ya familia, hivyo muda mwingi huwaacha watoto wao wakiwa na kaka ama dada zao na wakati mwingine bibi ama babu zao, ambao huwaachia kama ni viazi au uji hushindia huo hadi nyakati za jioni wanaporejea nyumbani na kuandaa chakula kingine ambacho hakina tofauti katika virutubishi kama walichokula mchana.

Tafiti zinahitaji jitihada zaidi kumaliza tatizo la njaa iliojificha

Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Kim, katika mkutano wake na mawaziri wa fedha kutoka mataifa mbalimbgali uliofanyika mwaka 2016 nchini Marekani alisema kuwa, asilimia 43 ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanaokadiriwa kufikia milioni 250 katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati wamedumaa.

Master zum Themenheader Kann Afrika den Hunger stillen?
Viazi vitamu vikivunwa shambani.Picha: AFP/Getty Images

Alisema watoto hao wanakabiliwa na utapiamlo mkali, unaosababishwa  na umasikini pamoja na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa kupata lishe bora kwa wanawake na watoto, hasa walio chini ya umri wa miaka mitano.

Kwa nchini Tanzania  utafiti uliofanywa na taasisi ya lishe (TFNC) kwa kushirikiana na ofisi ya taifa ya takwimu (NBS) kuhusu afya na viashiria vya malaria wa mwaka 2015-2016  unaonesha kuwa tatizo la udumavu linakabili zaidi wanawake walio katika umri wa kuzaa na watoto chini ya miaka mitano.

Utafiti huo unaonesha kuwa mkoa wa Rukwa unaongoza kuwa na watoto wengi wenye udumavu kwa kiwango cha asilimia 56 ukifuatiwa na mkoa wa Njombe kwa asilimia 49, Ruvuma asilimia 41, Iringa asilimia 42 na Kagera 42.

Kiuhalisia mikoa hii kwa nchini humo ndio inayoongoza kwa uzalisaji wa chakula hata hivyo ndio inayoonoza kuwa na kiwango cha juu kuwa na hali ya udumavu.

Mkopi anasema matokeo ya utafiti huo yanadhihirisha bado kuna kazi kubwa ya kupambana na  changamoto ya lishe duni inayosababisha  udumavu, uzito pungufu, upungufu wa damu na ukondefu.

Mapambano dhidi ya  njaa iliojificha.

Tatizo la udumavu katika nchi linawaleta pamoja wadau wa masuala ya lishe kwa kuweka mipano na mikakati inayoweza kutekelezeka kuanzia katika ngazi ya familia ili kuepuka udumavu na kutokomeza njaa iliojificha katika kaya.

Meneja wa mradi wa kapu lishe unaoonozwa na kituo ca kimataifa cha viazi lishe (CIP), Hilda Munyua  anasema  tafiti zimewafanya kuingia katika mradi huo ili kupambana na udumavu kwa uwiano sawa wa mijini na vijijini, ambapo wakulima wananweza kupanda mbegu zilizo na virutubiso vinavyohitajika mwilini.

"Mama akikosa afya bora atapata watoto walio na afya dhoofu, lakini na mtoto anapopata udumavu inakuwa ni Athari kubwa sababu ubongo wake unakuwa haujakomaa vilivyo anakuwa na uwelewa duni, sababu ya udumavu na unaweza ukaongea nae anakuangalia tu hata darasani hataweza kufanya vizuri.

Südsudan Hunger Symbolbild
Utapiamlo na udumavu ni matatizo yanayoikabili Tanzania.Picha: Getty Images/AFP/A. Gonzales Farran

"Katika mradi wetu tunasisitiza wakulima kuwa na mbegu zenye virutubiso vya kutosa sababu atapanda na atakula atauza chakula bora na wengine watapata pia, hii itasaidia kupambana na njaa iliojificha.”

Hata hivyo katika vituo vya afya kwa mijini hali inaonekana kuwa ni nzuri sababu wahudumu wamekuwa wakitoa darasa la lishe bora kwa wananwake wajawazito na watoto hatua ambayo imeleta mapinduzi makubwa katika lishe kwa wanawake na watoto.

Chiku Saalim ambae mwanae ana mwaka mmoja na nusu ameiambia DW kuwa "lishe kwa mtoto wangu ni jambo la kwanza sababu najua akipata maradhi sitaweza kufanya lolote, sitaweza kufanya kazi kumpatia mahitaji yake, atakumbwa na maradhi huku baya zaidi ikiwa ni udumavu,” alisema Chiku na kuongeza kuwa;

"Nimeweka utaratibu maalum wa chakula cha mwanangu, kwa mfano Jumatatu asubuhi akiamka, namlisha uji wa lishe, kisha analala tena, ikifika mchana nampatia parachichi, ndizi, na kiini cha yai la kienyeji ambavyo nakuwa nimeviandaa na kuvisaga kwa pamoja.

"Lakini inapofika  sisi (watu wazima) tunapokula chakula cha mchana unakuta na yeye analilia, basi namlisha japo kidogo, si sana…inapofika saa kumi jioni huwa tayari nimemuandalia chakula cha maharage au choroko ambacho huchanganywa kwa nazi au karanga na kusagwa kwa pamoja,” anasema.

Chiku anasema pamoja na hayo bado huzingatia kuhakikisha anamnyonyesha mwanawe ipasavyo na kumpatia maji ya kunywa ambayo anakuwa ameyachemsha yeye mwenyewe na kuyahifadhi vizuri nyumbani.

Maazimio ya serikali kumaliza njaa iliojificha.

Katika gazeti la mtandao la wizara ya afya maendeleo ya jamii jinsia, wazee na watoto naibu waziri Dokta Faustine Ndugulile anasema: "Zaidi ya asilimia 35 ya vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini vinachangiwa na matatizo ya lishe duni na katika kipindi cha mwaka 1992 hadi 2015/16 vimepungua kutoka 149 hadi 67 kwa kila vizazi hai 1000.

Hawkers of boiled maize in Tanzania at work
Mahindi ni chakula chenye wanga kwa wingi.Picha: DW/S. Khamis

"Udumavu umepungua kutoka asilimia 49.7 hadi 34.4 kwa upande wa ukondefu (uzito kwa urefu) kutoka asilimia 7.8 hadi 4.5  kwa upande wa uzito pungufu (uzito kwa umri)  kutoka asilimia 25.1 hadi 13.7. Vilevile mwanamke 1 kati ya 10 ana uzito pungufu wakati asilimia 18 wana uzito mkubwa na asilimia 10 wanakiribatumbo.”

Naibu waziri Huyo aliahidi kuwa watajipanga katika kutoa elimu ya afya kwa umma na kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kumaliza tatizo la udumavu.

Nini kifanyike kupambana na njaa iliojificha?

Shabaha ya shirika la afya duniani WHO ifikapo mwaka 2025 ni kwa kupunuguza kwa idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano waliodumaa kwa nchini Tanzania kwa asilimia 40. Hivyo ni muhimu kwa jamii ya Watanzania kuzingatia lishe bora kwa watoto, wajawazito na  wanawake walio katika rika la kuzaa.

Jean Claude Robyongo, mkuruenzi wa shirika la mbegu la kimataifa la CIAT anasema "lazima jamii ione umuimu wa afya zao na watoto, ambao ni tafa la kesho kwa kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anajiuliza alichokula kinakwenda kutengeneza nini au kinaboresha nini katika mwili wake na watoto wake, tukiwa na utamaduni huo hata walimu shuleni hawatapata tabu kubwa kusomesha watoto wetu.

"Utamaduni huo utasaidia pia watoto watakapokuwa watu wazima kuendeleza katika familia zao, lakini tunajikumbusha kuwa chakula ni tiba tunakula ili kuifanya miili yetu iwe na nguvu, tuweze kufikiri na kutoa maamuzi mazuri na  tuwe na afya njema, tukielewa kwa pamoja tutaacha kula sababu ya kushiba.”

Mwandishi: Hawa Bihoga

Mhariri: Iddi Ssessanga