1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asasi za kiraia zatakiwa kutoa elimu ya kura kwa wananchi

Hawa Bihoga18 Septemba 2019

Tanzania: Tume ya Taifa ya uchaguzi imezitaka asasi za kiraia, kutohesabu kiwango cha wapiga kura waliohudhuria katika vituo vya kupigia kura, badala yake wazingatie kura zilizoharibika na kutoa zaidi elimu kwa umma.

https://p.dw.com/p/3Pogi
Tansania Wahlen
Picha: Reuters/S. Said

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Tanzania NEC imezitaka asasi za kiraia nchini humo, kutohesabu kiwango cha wapiga kura waliohudhuria katika vituo vya kupigia kura na kujipongeza badala yake wazingatie kura zilizoharibika na kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa umma. Ushauri huo umetolewa katika kikao cha asasi za kiraia zinazohusika na masuala ya vijana kilichofanyika leo mjini Dae es Salaam.

Mwaka 2019 mwezi Novemba raia wa Tanzania watapiga kura kuchagua serikali za mitaa zenye jukumu la kikatiba la kupeleka madaraka kwa wananchi na kuwahusisha katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo. Mwaka mmoja baadaye,  2020 utafanyika uchaguzi mkuu wa rais na wabunge.

Ni kwa ajili hii asasi za kiraia zaidi ya ishirini zinazoshughulikia masuala ya vijana nchini humu kuungana kwa lengo la kutoa elimu kwa wapiga kura vijana ili kuweza kutekeleza ipasavyo zoezi hilo la kikatiba na kidemokrasia.

Katika mkutano uliozileta pamoja  asasi hizo kuweka ajenda zitakazopewa kipaumbele katika zoezi zima la kutoa elimu ya mpiga kura kijana, tume ya taifa ya uchaguzi imewataka wagombea kutoridhika na kiwango cha wapiga kura waliohudhuria katika vituo vya wapiga kura badala yake kujipima katika idadi ya kura zilizoharibika, kwani hiyo ni ishara ya elimu kuhitajika zaidi. Huyu ni Daniel Kasokola, mkurugenzi msaidizi wa idara ya Habari na Elimu ya mpiga kura katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania.

Sehemu ya ajenda ambazo zinatajwa kupigiwa chapuo na asasi za kiraia kwa kijana ni pamoja na masuala ya ajira, tekonolojia na ubunifu, uzingatiwaji wa haki za binadamu, siasa, afya pamoja na masuala ya demokrasia. Hussein Malele mkurugenzi mtendaji wa asasi ya MULIKA ameiambia DW kuwa hayo ni muhimu kujitokeza katika ajenda yao kwa kijana..

Hadi sasa tume ya taifa ya uchaguzi ipo katika zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura, likibeba kauli mbiu Kadi yako, kura yako nenda kajiandikishe.