1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TAMWA yazungumzia rushwa ya ngono kwa wanahabari wa kike

Hawa Bihoga11 Septemba 2018

Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania TAMWA kimesema kukosekana kwa sera madhubuti kuhusu masuala ya ngono katika mazingira ya kazi kumechangia kuongezeka kwa visa vya rushwa ya ngono katika vyombo vya habari.

https://p.dw.com/p/34f1p
Hawa Bihoga  Edda Sanga
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Eda Sanga akuzungumza na mwandishi wa DW Hawa Bihoga jijini Dar es Salaam, Septemba 11, 2018.Picha: Tamwa

TAMWA imesema hayo ikiwa ni siku chache baada ya kituo cha sheria na haki za binadamu kutoa ripoti yake ya nusu mwaka inayoelezea hali ya haki za binandamu nchini Tanzania ambapo mbali na mambo mengine imeonesha kuongezeka kwa visa vya rushwa ya ngono kwa waandishi habari wananawake.

Mkurugenzi mtendaji wa chama cha waandishi wa habari wanawake Eda Sanga ameiambia DW kuwa, licha ya baadhi yao kukumbwa na kadhia hiyo ambayo inashusha utu wa mwanamke na kukiuka misingi ya binadamu, ukosefu wa sera ya usimamizi wa masuala ya ngono katika vyombo vya habari bado ni changamoto kubwa katika kukabiliana na tatizo hilo.

Hata hivyo tafiti mbalimbali za kidunia zinaonesha kuwa takriban asilimia arobaini na moja ya wanawake wanahababri na wasanii wanakumbana na visa vya kingono katika mazingira ya kazi, huku wananume ni asilimia ishirini na mbili, hii ikionyesha kuwa wanahabari wananwake wanaathirika zaidi kuliko wanaume.

Tansania Debatte über Media gegen Fake News
Baadhi ya waandishi habari wa kike wakiwa katika mjadala kuhusu habari za uongo ulioandaliwa na DW jijini Dar es Salaam, Tanzania, Oktoba 27, 2017.Picha: DW/E. Boniphace

Vichocheo vya rushwa ya ngono miongoni mwa wanahabari

Eda Sanga anaongeza kuwa kutokana na uzoefu wake katika tasnia ya habari, anasema kutokuwa na mapenzi ya dhati ya tasnia hiyo ni sehemu ya kichocheo cha kuongezeka kwa matukio ya rushwa ya ngono katika vyumba vya habari, ikiwemo na utendaji duni wa baadhi ya waathirika wa visa hivyo vya kingono.

Katika hili waandishi wa habari wanawake wanasema kuwa manyanyaso ya kingono katika vyumba vya habari bado yanashuhudiwa, hata baadhi hushushwa kiwango cha utendaji kazi wao kutokana na wao kukataa kutoa ngono, huku wengine wakidai kuwa wakati wa kuomba ajira hili linajitokeza zaidi.

Hili linatajwa kujitokeza katika vyombo vya habari mbalimbali ulimwenguni hata baadhi ya wanawake ambao wamekumbana na kadhia hiyo kuanzisha kampeni mbalimbali ambazo zinapinga vikali rushwa ya ngono na udhalilishaji wa kingono kwa waandishi wa habari wanawake katika vyombo vya habari, ikiwemo kampeni mashuhuri iliokwenda kwa jina la kimombo "me too” inayotajwa kuleta uthubutu wa kuzungumza kadhia za kingono kwa wanahabari wanawake kwa uwazi.

Mwandishi: Hawa Bihoga Dw Dar es salaam

Mhariri:Josephat Charo