1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tamasha la muziki wa rock kuendelea baada ya kitisho

3 Juni 2017

Tamasha kubwa la muziki Ujerumani la "Rock am Ring" litaendelea kama ilivyopangwa baada ya kutibuliwa na hofu ya uwezakano wa "shambulio la kigaidi" ambalo waandalizi wamesema imethibitika kuwa halina msingi.

https://p.dw.com/p/2e5hK
Musikfestival Rock am Ring
Picha: picture-alliance/dpa/T. Frey

Tamasha kubwa kabisa la muziki nchini Ujerumani linalotambulika kwa jina la "Rock am Ring" litaendelea kama ilivyopangwa baada ya kutibuliwa na hofu la uwezakano wa "shambulio la kigaidi" ambalo waandalizi wa tamasha hilo wamesema imethibitika kuwa halina msingi.

Polisi imeliambia shirika la habari la AFP kwamba msako uliofanyika katika mji wa kusini magharibi wa Koblenz kwa tamasha hilo la siku tatu umemalizika na kwamba muziki unaopigwa moja kwa moja wakati wa tamasha hilo utaanza tena saa moja na nusu usiku.

Waandalizi wamesema baada ya misako kadhaa mikubwa katika eneo hilo zima la tamasha,hofu ya kuwepo hatari kwa yakini haikuweza kuthibitishwa na polisi imeruhusu kuanza tena kwa tamasha hilo.

Hapo jana jioni watu waliondolewa katika tamasha hilo baada ya polisi ya Koblenz kusema wamevitia mikononi vitu vyenye kutowa mwanga ambao hauondowi uwezekano wa tishio la kigaidi.

Watatu walishikiliwa

Festival Rock am Ring - Nach der Terrordrohung
Washabiki wa tamasha la muziki la Rock am Ring.Picha: Reuters/W. Rattay

Polisi ilisema watu watatu waliokuwa wakituhumiwa kuwa wanachama wa kundi moja la Masalafist katika jimbo la jirani la Hesse walitiwa kizuizini lakini wakaachiliwa Jumamosi.

Msemaji wa polisi Wolfgang Fromm amesema "Mtu mmoja ambaye hana asili ya Ujrumani na anayejulikana kwa kuwa na mahusiano na mtandao wa kigaidi wa Kiislamu alikuwa na ruhusa ya kuingia maeneo ya maandalizi ya tamasha hilo.Watu hao watatu walikuwa wamekodiwa kuweka vizuizi vya usalama katika eneo hilo.

Usalama ulikuwa tayari umeimarishwa katika eneo hilo kwa kuongeza wafanyakazi zaidi 1,200 baada ya kutokea kwa mripuko wa bomu huko Manchester Uingereza hapo Mei 22 baada ya onyesho la muziki la mwimbaji wa Marekani Ariana Grande.

Uamuzi watetewa

Musikfestival Rock am Ring - Pressekonferenz mit Roger Lewentz
Roger Lewentz waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Rhineland- Palanatinate akizungumza na waandishi wa habari.Picha: picture-alliance/dpa/T. Frey

Waziri wa mambo ya ndani wa eneo hilo Roger Lwentz ameutetea uamuzi wa kuwaondowa watu katika tamasha hilo kwa kusema"Hatuwezi kubahatisha katika suala la hatari."

Ratiba ya mwaka jana ya tamasha hilo la muziki la "Rock am Ring" ilitibuliwa kutokana nav dhoruba kali ambapo watu kadhaa walijeruhiwa kutokana na radi.

Ujerumani inaendelea kuwa katika hali ya tahadhari baada ya shambulio la miganaji wa jihadi katika soko la Krismasi tarehe tisa Disemba mjini Berlin.Raia wa Tunisia Anis Amri mwenye umri wa miaka 29 aliliteka nyara lori na kumuuwa dereva wake Mpoland kabla ya kulibamiza kwenye soko lililofurika watu na kusababisha vifo vya watu 11 na kujeruhi wengine wengi.

Takriban watu 90,000 wanatarajiwa kuhudhuria tamasha hili ambalo linamalizika Jumapili.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri. Sudi Mnette