1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taliban yazuia watu kuondoka nchini Afghanistan

Babu Abdalla19 Agosti 2021

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza amesema hatma ya Afghanistan baada ya vita vya miaka 20 imetoa taswira kuwa azimio la mataifa ya Magharibi nchini Afghanistan sasa linaonekana kuwa dhaifu na maadui wake wakuu.

https://p.dw.com/p/3zA7I
Afghanistan | Taliban Kämpfer patrouillieren  durch die Straßen von Kabul
Wapiganaji wa Taliban wakishika doria katika eneo la Wazir AkbarPicha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amesema hatma ya Afghanistan baada ya vita vya miaka 20 vilivyoongozwa na Marekani imetoa taswira kuwa azimio la mataifa ya Magharibi nchini Afghanistan sasa linaonekana kuwa dhaifu na maadui wake wakuu kama vile Urusi, kauli yake ameitoa wakati maelfu ya Waafghani wakiendelea kuikimbia nchi hiyo kwa kuhofia utawala wa Taliban.

Vita nchini Afghanistan vimegharimu mabilioni ya dola lakini licha ya hayo, kundi la Taliban sasa limechukua usukani wa kuliongoza taifa hilo huku mataifa ya magharibi yakiendelea na juhudi za kuwahamisha wafanyikazi wake pamoja na raia wengine wa Afghanistan kutoka uwanja wa ndege wa Kabul.

Soma zaidi: Licha ya kukosolewa, Biden atetea uamuzi wa kuondoa vikosi Afghanistan

Waziri wa Ulinzi wa Uingereza Ben Wallace amesema ana wasiwasi juu ya utawala wa Taliban na ombwe lililoachwa na mataifa ya Magharibi baada ya kuondoa vikosi vyake vya usalama. Wallace anasema kuondoka kwa vikosi hivyo vya usalama kutafungua mwanya kwa makundi ya kigaidi kama vile al-Qaeda kupata nafasi ya kujiimarisha tena nchini humo.

"Kitu kinachonitia hofu ni kwamba sasa tuna mfumo mpya wa maisha ambapo kufeli kutatua matatizo kunachukuliwa na maadui zetu kama udhaifu. Nafahamu kuwa hauwezi kupata suluhu ya mara moja ya hali nchini Afghanistan, na tunachofanya sasa kutakuwa na athari ya kihistoria kwa miaka mengine ijayo."

Deutschland, Frankfurt | Ankunft Evakuierter aus Afghanistan
Mahmud Sadjadi akiwasili nchini Ujerumani akitokea AfghanistanPicha: Frank Rumpenhorst/dpa/picture alliance

Waziri huyo wa Ulinzi wa Uingereza ameongeza kuwa, makundi ya itikadi kali duniani kote yatapata hamasa na kuwatia moyo ya kujiimarisha zaidi kufuatia ushindi wa kundi la wanamgambo la Taliban.

Wapiganaji wa Taliban wameshika doria na kuwakagua watu wanaoingia katika uwanja wa ndege wa Kabul leo Alhamisi, wakati kukiwa na wasiwasi kuwa wanawazuia Waafghani kuondoka nchini humo.

Marekani imesema imeshangazwa na hatua ya Taliban ya kuwazuia watu kuondoka nchini humo licha ya kutoa ahadi ya kuwaruhusu Waafghani waliofanya kazi kwa ushirikiano na mataifa ya Magharibi na washirika wake kuondoka.

Soma zaidi: Kipi kinafuata Afghanistan baada ya kuibuka tena kwa Taliban?

Naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani Wendy Sherman amesema anatarajia kuwa Taliban itatimiza ahadi yao ya kuwarahusu raia wote wa Marekani pamoja na Waafghani wanaotaka kuondoka bila ya kuwawekea vikwazo vyovyote.

Maelfu ya watu wanajaribu kuikimbia nchi hiyo wakihofia utawala wa Taliban. Hapa Ujerumani, watu waliowasili katika uwanja wa ndege wa Frankfurt wakitokea Afghanistan wameelezea matukio ya kutisha waliyoyaona nchini Afghanistan. Mahmud Sadjadi ambaye ni raia wa Ujerumani, amesema ameona maiti kadhaa barabarani na kusikia milio ya risasi mjini Kabul, na kwamba hali ni mbaya sana.

Tangu siku ya Jumanne, jeshi la Ujerumani limekuwa likiwahamisha watu kutoka mjini Kabul.