Taliban wayasifu mazungumzo ya Oslo | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.01.2022
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Taliban wayasifu mazungumzo ya Oslo

Mazungumzo kati ya kundi la Taliban na wanadiplomasia wa nchi za Magharibi yameingia siku yake ya tatu na ya mwisho hii leo huko mjini Oslo Norway.

Mazungumzo hayo yamelenga kwa kiasi kikubwa juu ya hali ya kibinadamu nchi Afghanistan. Mengi zaidi anaarifu Tatu Karema katika taarifa ifuatayo.

Mazungumzo hayo ya Oslo yalianza siku ya Jumapili yakifanyika baina ya Taliban na wanachama wa mashirika ya kiraia ya Afghanistan na kisha Jumatatu yakafuatia na mazungumzo mapana yaliyoshirikisha pande mbali mbali pamoja na wanadiplomasia wa nchi za Magharibi kutoka Umoja wa Ulaya,Marekani na Uingereza Ufaransa, Italia na mwenyeji Norway.

Soma Zaidi: Taliban na Magharibi waijadili hali nchini Afghanistan

Mazungumzo na pande zote ikiwemo mashirika huru ya shughuli za kibinadamu ndiyo yanayotarajiwa kufanyika leo Jumanne.

Mikutano hiyo inayofanyika faragha inaendelea kwenye hoteli iliyoko milimani katika mji mkuu wa Norway-Oslo na inatarajiwa kugusia kila kitu kuanzia masuala ya elimu mpaka msaada wa kibinadamu bila ya kuliacha suala la kutaka watu wote wajumuishwe.

Juhudi hizi zimekuja katika wakati muhimu sana kwa Afghanistan ambayo inashuhudiwa majira ya baridi kali.Nchi hiyo pia iko katika hali mbaya baada ya kuondoka wanajeshi wa Marekani na kundi la Taliban kutwaa madaraka ya kuiongoza.

Pakistan Flüchtlinge Afghanistan humanitäre Krise Symbolbild

Raia nchini Afghanistan ambao wamekimbia makazi yao wakiwa wamejipanga msitari wa kupokea misaada wa chakula

Mashirika ya misaada yaonya kuhusu kitisho cha njaa Afghanistan.

Mashirika ya misaada na yale ya kimataifa yanakadiria kwamba kiasi watu milioni 23 ambao ni zaidi ya nusu ya idadi jumla ya watu wa taifa hilo wanakabiliwa na hali njaa kali na wengine takriban milioni 9 wako ukingoni kukabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula.

Watu wamejikuta wakiuza mali zao kununua chakula,wakichoma samani zao kwa ajili ya kuwasha moto wa kuleta joto na kujikinga na baridi na wakati mwingine hata kuwapiga bei watoto wao. Umoja wa Mataifa umefanikiwa kutowa fedha kiasi na kuruhusu utawala wa Taliban kutumia kuagiza bidhaa kutoka nje ikiwemo umeme.Wajumbe wa Taliban kwenye mazungumzo ya Oslo wanataka fedha za nchi yao kiasi dola bilioni 10 zinazozuiliwa na Marekani na nchi nyingine za Magharibi ziachiliwe.

Japokuwa nchi za Magharibi huenda zikatanguliza mbele kwenye egenda zao   suala la haki za wanawake  na wasichana. Kadhalika suala jingine linalopewa kipaumbele na nchi hizo ni lile la kuitaka serikali ya Taliban kugawana madaraka na  na makundi ya waliowachache pamoja na makundi ya kidini.

Pamoja na kwamba Norway na washirika wake wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO hawautambui utawala unaoongozwa na Taliban nchini Afghanistan, ilionyakua madaraka kwa nguvu mwaka jana lakini unayatazama mazungumzo haya kuwa muhimu na hasa kwa kuzingatia ukubwa wa mgogoro wa nchi hiyo.

Soma Zaidi: Nchi za Magharibi hazijaridhishwa na serikali ya Taliban

Wajumbe wa Taliban waliokwenda Oslo wameiita hatua ya kufanyika mkutano huu kwamba yenyewe ni mafanikio tosha ingawa jumuiya ya kimataifa  imesisitiza kwamba ikiwa Taliban linataka kupata msaada linapaswa kwanza kuheshimu haki za binadamu.