1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Taliban wanazidisha udhibiti kusini wa Afghanistan

Saleh Mwanamilongo
3 Agosti 2021

Jeshi la Afghanistan limewataka raia kuondoka kwenye mji wa Lashkar Gah unaodhibitiwa na wapiganaji wa Taliban,huku likijiandaa kuanzisha operesheni kabambe.

https://p.dw.com/p/3yTzM
Afghanistan Konflikt Taliban Terrorismus
Picha: Rahmat Gul/AP/picture alliance

Amri hiyo imetolewa kufuatia mapigano makali yaliyodumu siku tatu. Wapiganaji Wataliban walidhibiti maeneo kadhaa ya Afghanistan tangu majeshi ya kigeni yalipoanza kuondoka nchini humo mwezi Mei. Hivi sasa wapiganaji hao wanajaribu kuudhibiti mji wa Lashkar Gah, mji mkuu wa jimbo la Kusini la Helmand.

Jeshi laapa kuukinga mji wa Lashkar Gah

Jenerali Sami Sadat, kamanda wa kitengo cha 215 cha jeshi la Afghanistan,amewambia wakaazi wa mji huo kuyahama makaazi yao haraka iwezekanavyo.

Amesema watawasaka Wataliban mahala popote walipo na hawatoacha mpiganaji yeyote wa kundi hilo akiwa hai.

''"Natoa ahadi kwamba jeshi la Afghanistan na vikosi vyote vya usalama vitawashinda wapiganaji wa Taliban na Tumedhamiria hata mpiganaji mmoja ataingia katika eneo la Lashkar Gah atauwawa, na hata kama wataingia 1,000 wote watauwawa.'' alisema Sadat.

Mapema viongozi walitangaza kwamba wanamgambo walidhibiti vituo vyote vya redio na televisheni vya mji wa Lashkar Gah, wakiacha kituo kimoja pekee kinacho waunga mkono kupeperusha matangazo ya kiislamu.

Umoja wa Mataifa unaelezea wasiwasi wake kuhusu usalama wa raia kufuatia mapigano hayo. Kikosi cha usaidizi cha Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan,UNAMA,kimetoa mwito wa usitishwaji mapigano kwenye maeneo ya miji.

Kurejea kwenye meza ya mazungumzo

 Umoja wa mataifa wahimiza pande mbili kurejea kwenye meza ya mazungumzo
Umoja wa mataifa wahimiza pande mbili kurejea kwenye meza ya mazungumzoPicha: Karim Jaafar/AFP

T.S. Tirumurti, balozi wa India kwenye Umoja wa Mataifa,ambaye nchi yake inaongoza mwezi huu wa Agosti baraza la usalama amezitaka pande mbili kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

''Machafuko yote yanatakiwa kukomeshwa. Na ushirikano wowote na ugaidi wa kimataifa unatakiwa kusitishwa. Na hatuwezi kubali magenge ya kigaidi kurejea tena nchini Afghanistan.'' alisema Tirumurti.

Sefatullah, Mkuu wa kituo cha redio cha ''Sukon Radio'' kwenye mji huo wa Lashkar Gah amesema mapambano makali yalishuhudiwa asubuhi ya leo.

Amesema ndege za kivita za Marekani na Afghanistan zilishambulia maeneo yanayokaliwa na wanamgambo wa Taliban. Sefatullah amesema mapigano yaliendelea karibu na gereza na kwenye jengo la makao makuu ya idara ya upelelezi na polisi.

Jeshi la Afghanistan lazidiwa nguvu

Siku za hivi karibuni, jeshi la Marekani lilizidisha mashambulizi yake ya anga nchini Afghanistan  ili kuzuwiya Wataliban kusonga mbele.

Kupotezwa kwa mji wa Lashkar Gah ni pigo la kimkakati na la kisaikolojia kwa serikali ya Afghanistan, ambayo ilitangataza kuhifadhi mji huo kwa garama yoyote ile, baada ya kupoteza udhibiti wa maeneo kadhaa ya mashambani.

Mjini Herat, mji mwingine uliozingirwa, mamia ya raia walikuwa wakiimba ''Allahu Akbar'' (Mungu ni mkubwa) kwenye paa za nyumba zao baada ya jeshi kurejesha nyuma shambulizi la wapiganaji wa Taliban.

Mafisawaserikali ya Afghanistan walisema vikosi vya nchi hiyo viliwarejesha nyuma wanamgambo kwenye maeneo kadhaa,ukiwemo uwanja wa ndege wa Herat ambao ni muhimu kwa ugavi wa vifaa.