1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taleban wajizatiti jimboni Swat

4 Mei 2009

Uongozi nchini Pakistan umetisha kuwachukulia wapiganaji wa Taleban hatua za kijeshi endapo wataendelea kukiuka amri ya kutotoka nje nje iliyotangazwa katika mji wa Mingora ulio jimboni Swat.

https://p.dw.com/p/HjNy
Ramani ya Jimbo la Swat(njano) la PakistanPicha: GFDL / Pahari Sahib


Kwa upande wao wapiganaji wa Taleban waliojihami wanaripotiwa kushika doria bila uwoga wowote.Yote haya yanatokea baada ya makubaliano ya muda ya kusitisha vita kufikiwa miezi mitatu iliyopita.Wakati huohuo Rais Barack Obama wa Marekani anatarajiwa kukutana na viongozi wa Pakistan na Afghanistan ifikapo Jumatano kwa lengo la kujadili mkakati wa kupambana na wapiganaji wa Al –Qaeda.



Uongozi wa Pakistan unakabiliwa na mivutano wakati ambapo Marekani inaushinikiza kuongeza muda wa operesheni ya kuwafurusha wapiganaji wa Taleban.Kundi la Taliban kwa upande wao limepinga vikali hatua ya kuundwa mahakama za rufaa za kiislamu kwa ajili ya kuusambaratisha uasi huo.Mahakama hizo za sharia zilianzishwa katika jimbo la kaskazini magharibi la Swat.Kwa mujibu wa wadadisi makubaliano hayo yaliyofikiwa miezi mitatu iliyopita sasa yanatetereka.


Taliban in Pakistan
Wakazi wa eneo la Mingora jimboni SwatPicha: picture alliance / landov

Serikali ilitangaza muda wa kutotoka nje katika mji mkuu wa jimbo hilo wa Mingora ambako wapiganaji wa Taleban wanaripotiwa kushika doria bila uwoga wowote.

Makubaliano hayo yaliyofikiwa mwezi wa Februari yaliidhinishwa na rais Asif Ali Zardari mwezi uliopita yalikosolewa vikali nchini humo vilevile na jamii ya kimataifa.Wakosoaji walidai kuwa hatua hiyo zaidi itawatia nguvu wapiaganaji wa Taleban badala ya kuleta tija yoyote.


Hofu na wasiwasi huo ulizidi kutanda pale wapiganaji wa Taliban walipoishambulia wilaya jirani ya Buner.Katika kipindi cha siku kumi zilizopita ndege za kijeshi pamoja na wanajeshi wa nchi kavu wamekuwa wakiwasaka wapiganaji wa Taleban ambao wanaripotiwa kukimbia katika maeneo ya mbali zaidi mikoani Dir ya Kaskazini na Buner.

Kwa mujibu wa Waziri wa Misitu anayetokea eneo hilo Wajid Ali Khan,wapiganaji wa Taliban wanakiuka makubaliano yaliyofikiwa kwa kushika doria na huenda serikali ikalazimika kuwashambulia endapo hawatoridhia kusitisha operesheni zao kwa amani.


Neue Militäroffensive gegen Taliban in Pakistan
Mwanajeshi anayeshika doria katika eneo la Dir ya KaskaziniPicha: picture-alliance/ dpa

Kwa upande mwengine Rais Barack Obama wa Marekani anatarajiwa kukutana na viongozi wa Pakistan na Afghanistan ifikapo Jumatano kutokana na hali iliyopo.Mkakati mpya wa Marekani wa kupambana na wapiganaji wa Taliban na Al Qaeda wanaoendesha operesheni zao Afghanistan na Pakistan haujapokelewa vizuri na jamii ya kimataifa wala katika nchi husika.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa viongozi hao kukutana ana kwa ana wakiwa na azma ya kujadili mkakati huo mpya.Hata hivyo Rais Obama ataweza kupata fursa ya kuwasilisha hisia zake kuhusu masuala ya rushwa na ufisadi pamoja na uongozi mbaya.Changamoto kubwa ni kuishawishi Pakistan kulipa uzito tishio la uasi kadhalika kuwazuia wapiganaji wa Taleban kuendeleza operesheni zao dhidi ya Afghanistan wakiwa nchini mwao.Kauli hizo zinaungwa mkono na Waziri wa Ulinzi wa Marekani Robert Gates aliyesema kuwa ''Kuvunjika kwa makubaliano ya kusitisha vita katika jimbo la Swat pamoja na harakati za kuivamia Buner ni mambo yaliyoifungua macho serikali ya Pakistan.Nadhani viongozi wa pakistan wanalielewa hilo ila kuna haja yao wao kuwafahamisha raia wengine wa Pakistan.''


Wakati huohuo mlipuaji mmoja wa kujitoa muhanga amemshambulia meya wa Mehterlam ulio mji mkuu wa jimbo la Laghman pamoja na watu wengine watano.Shambulio hilo limesababisha vifo vya meya huyo,binamu yake,walinzi wawili na wanakijiji wawili kwa mpigo mmoja.

Shambulio hilo limethibitishwa na naibu gavana wa jimbo hilo Edayatullah Qalanderzai.Itakumbukwa kuwa Rais Hamid Karzai anapanga kuwania muhula wa pili katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka huu.Tayari Rais Karzai ameshajisali na kuwatangaza makamu wa rais wa sasa Karim Khalili pamoja na makamu wa rais wa zamani Qasim Fahim kuwa wagombea wake wenza.Uchaguzi huo umepangwa kufanyika ifikapo tarehe 20 mwezi Agosti.Wagombea wengine wamepewa muda wa wiki moja kujisajili. Hamid Karzai amekuwa madarakani tangu utawala wa Taleban kuangushwa mwaka 2001.



Mwandishi:RTRE/AFPE

Mhariri:Mohamed Abdulrahman