Takataka za kinuklea zasafirishwa kuelekea Gorleben | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.11.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Takataka za kinuklea zasafirishwa kuelekea Gorleben

Makotena yaliyotengenezwa maalum kwaajili ya kusafirishia takataka za kinuklea yanatarajiwa kuwasili Gorleben,baada ya kucheleweshwa kwa masaa kadhaa kutokana na maandamano ya wapinzani wa nishati ya kinuklea

Mwanaharakati amejitupa katika njia ya reli kuzuwia safari ya treni iliyosheheni takataka za kinuklea huko Dannenberg

Mwanaharakati amejitupa katika njia ya reli kuzuwia safari ya treni iliyosheheni takataka za kinuklea huko Dannenberg

Baada ya kuzuwiliwa kwa zaidi ya siku mbili na wanaharakati wanaopinga nishati ya kinuklea,msafara wa treni iliyosheheni makontena maalum ya takataka za kinuklea uliokuwa ukielekea katika bohari ya muda huko Gorleben hatimae umeondoka Dannenberg.

Polisi wamefanikiwa kuondowa vizuwizi pamoja na wanaharakati 4000 waliopiga kambi kwa zaidi ya saa 45 katika njia ya reli ambako treni hiyo ya makontena yaliyosheheni takataka za kinuklea ilikuwa ipite.Hata hivyo haijulikani lini makontena hayo yatawasili katika bohari ya muda huko Gorleben.Tangu jana usiku makontena hayo yaliyosheheni takataka za kinuklea yalikuwa yakipandishwa katika malori kwa msafara wa kilomita 20 za mwisho kati ya Dannenberg na bohari ya muda huko Gorleben.Polisi walikumbana na upinzani mkali wa wanaharakati wa shirika la ulinzi wa mazingira-Green Peace.Msemaji wa polisi Markus Scharf anasema tunanukuu::

"Wanaharakati wa Green-peace wametangulia na magari yao,wametupa vizuwizi vizito vizito katika njia ya reli na kujifunga navyo,Polisi ilibidi kwanza ipate njia ya kuyafikia magari yao,kutenga vizuwizi na baadae kuwafunguwa wanaharakati hao kwa msaada wa chombo maalum.Nijuavyo mie hakuna aliyejeruhiwa."

Ripoti za hivi punde zinasema makontena yaliyosheheni takataka za kinuklea yameshaanza kuondoka Dannenberg kuelekea Gorleben.Ikiwa hakuna machafuko yoyote yatakayotokea,basi makontena hayo yanaweza kuwasili leo mchana.

Milolongo ya magari ya polisi yanashindikiza malori yanayosafirisha takataka hizo masafa ya kilomita 20 zilizosalia.Malori hayo yanaendeshwa kidogo kidogo na kupita vijijini.Kwa mujibu wa vyombo vya habari hakuna machafuko yaliyotokea hadi sasa.

Wadadisi wanakubaliana msafara wa mwaka huu umechukua muda mrefu zaidi kuliko yote 11 mengine tangu takataka za kinuklea zilipoanza kupelekwa Ufaransa kusafirishwa katika kinu maalum cha La Hague mnamo mwaka 1995.Pia maandamano dhidi ya misafara hiyo hayajawahi kuwa makali kama mwaka huu.Ghadhabu za umma zinatokana hasa na uamuzi wa kurefusha muda wa vinu vya nishati ya kinuklea na uchunguzi unaoendelea kama bohari ya Gorleben itumike kama kituo cha mwisho cha kuhifadhia takataka za kinuklea.

Mwandishi:Gröning Lars/Hamidou Oummilkheir/dpa

Mpitiaji:Josephat Charo

 • Tarehe 09.11.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Q2Fq
 • Tarehe 09.11.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Q2Fq
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com