1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaTaiwan

Taiwan yawatafuta watu 18 waliokwama baada ya tetemeko

5 Aprili 2024

Vikosi vya uokoaji vya Taiwan vinaendelea na juhudi za kuwatafuta watu 18 waliokwama kwenye eneo moja la milimani baada ya tetemeko kubwa la ardhi kukipiga kisiwa hicho chenye utawala wake wa ndani siku ya Jumatano.

https://p.dw.com/p/4eRqa
Juhudi za uokoaji zikiendelea Taiwan
Juhudi za uokoaji zikiendelea Taiwan Picha: Tyrone Siu/REUTERS

Janga hilo la asili lilisababisha vifo vya watu 10 kwenye kaunti ya Hualien ambayo ina idadi kubwa ya watu. Pia liliwaacha mamia wengine wakiwa wamekwama kwenye mbuga moja ya wanyama iliyozingirwa na safu za milima.

Idara ya uokoaji ya kisiwa hicho imesema watu 18 bado wamekwama kwenye eneo hilo ikiwemo raia wa kigeni kutoka India, Canada na Australia.

Tetemeko la siku ya Jumatano lilikuwa na ukubwa wa 7.2 katika kipimo cha Richter na mitetemeko mingi midogo ilisikika pia baadaye kwenye kaunti hiyo ya Hualien na kwenye mji mkuu Taipei.

Kijiografia Taiwan inapatikana kwenye eneo lililo katika hatari ya kukumbwa na matetemeko ya ardhi. Janga kubwa kabisa lilitokea mwaka 1999 ambapo tetemeko lenye ukubwa wa 7.3 liliwaua zaidi ya watu 2,000.