1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taarifa za michezo

Mohammed AbdulRahman9 Novemba 2006

Bayern Munich yaanguka hadi nafasi ya tano katika ligi kuu ya Ujerumani-Bundesliga na nani atatawazwa bingwa wa Afrika Jumamosi katika mchuano kati ya Al Ahly ya Misri na Sfaxien ya Tunisia ?

https://p.dw.com/p/CHcz
Bayern wenye nyekundu katika mpambano dhidi ya Hannover 96. Hannover alishinda 1-0.
Bayern wenye nyekundu katika mpambano dhidi ya Hannover 96. Hannover alishinda 1-0.Picha: AP

Gumzo kuu huko Misri, Tunisia na kwengineko barani Afrika, ni mchuano wa duru ya pili ya fainali ya kombe la kilabu bingwa abarani humo, kati ya Al-Ahly ya Misri na Sfaxien Sportif ya Tunisia Jumamosi ijayo. Sfaxien imepania kulitwaa kombe hilo kufuatia matoke ya mchezo wake wa kwanza ya sare ya bao 1-1 mjini Kairo. Hivyo itahitaji kwenda sare ya bila kwa bila au kushinda kulinyakua kombe hilo. Tayari mlinzi wa Al Ahly wanaojulikana kama Mashetani wekundi wa Kairo,Wael Gomaa amekiri kwamba kilabu yao inakabiliana na shinikizo. Al Ahly inawania kuweka rekodi na kulitwaa kombe hilo kwa mara ya tano.

Iwapo itafanikiwa kushinda itakua imesawazisha rekodi ya mahasimu wao Zamalek ambao wameshalitwaa kombe hilo mara tano. Al-Ahly itasherehekea miaka 100 tangu kuundwa hapo mwakani na katika kipindi cha miaka 30 iliopita imetawala katika soka la nyumbani na barani Afrika. Ama Sfaxien itahakikisha kombe linabakia nyumbani ikizingatia ule usemi wa wahenga “ Mcheza kwao hutunzwa.” Lakini yote hayo tisa, la kumi ni kwamba muamuzi ni firimbi ya mwisho hapo Jumamosi.

Upande wa kimataifa, Manchester United ya England imekanusha ripoti kwamba kijana aliyejipatia sifa katika kandanda nchini Marekani Fredy Adu , ataanza mazoezi karibuni na miamba hiyo ya ligi kuu ya England. Taarifa ya Manchester Unioted kupitia mtandao wake, ilisema Adu hatoshiriki katika majaribio kwa sababu inaripotiwa amejihusisha pia na kilabu ya Atlantic ya Marekani. Adu mwenye umri wa miaka 17 alisemekana angejiunga na Manchester United kwa mazoezi ya majaribio tarehe 18 mwezi huu kwa muda wa majuma mawili. Kwa wakati huu mshambuliaji huyo amesajiliwa na DC United ya Marekani na akisemekana kuwa na hamu ya kulisakata dimba barani Ulaya.

Katika ligi ya Ujerumani Bundesliga, Bayern Munich jana usiku ikliaibika katika uwanja wa nyumbani ilipojikuta ikilazwa bao 1-0 na Hannover , miongoni mwa timu tatu za mwisho katika Bundesliga zinazokabiliwa na hatari ya kushuka daraja. Kutokana na kipigo hicho kisichotazamiwa, Bayern sasa iko nafasi ya tano katika msimamo wa ligi hiyo. Werder Bremen bado iknaongoza ikiwa na pointi 23 na leo itakua uwanajani kuchuana na Borussia Dortmund, wakati Bayern Munich itajaribu tena kesho itakapokua mgeni wa Bayer Leverkusen. Stuttgart iko nafasi ya pili kiwa na pointi 21 na Schalke iko nafasi ya tatu kwa pointi 20. Kutokana na kushindwa huko jaa, Bayern Munich sasa ina pointi 17 ikitanguliwa nafasi ya nne na Hertha Berlin kwa wingi wa magoli.

Katika ringi ya mabondi, Bingwa zamani wa uzito wa juu Mohammad Ali, atarudi tena katika ukumbi maarufu wa Madison Square Garden Jumamosi, ikiwa ni miaka 35 tangu lile pambano lake la kukata na shoka dhidi ya Joe Frasier. Lakini safari hii itakua sio kuzitwanga bali kumuangalia binti yake laila Ali akizipiga dhidi ya mpinzani wake Shelley Burton.

Laila mwenye umri wa miaka 28 na atakayelitetea taji lake la ubingwa wa dunia wa uzito wa kati- super middle -kwa wanawake, ni mdogo miongoni mwa binti zake wawili na mkewe wa tatu Veronica, kabla ya kuachana. Ali ana jumla ya watoto 9. Laila ameshashinda ndondi zote 22 alizopigana hadi sasa na 19 kati ya hizo aliweza kumaliza udhia na mapema.