1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yalaani Trump kuitambua Golan kuwa sehemu ya Israel

Angela Mdungu
22 Machi 2019

Syria imelaani kauli ya Rais Donald Trump, kuwa ni wakati wa kuitambua milima ya Golan kuwa sehemu ya Israel na kuapa kwamba italirejesha eneo hilo kwenye umiliki wake kwa kutumia kila njia iliyonayo.

https://p.dw.com/p/3FUhs
Israel - Syrien Golan-Höhen
Picha: Getty Images/AFP/J. Eid

Wazo hilo la Rais Trump limezua mwelekeo mpya katika sera za Marekani juu ya hali ya mgogoro katika eneo la Milima ya Golan lililodhibitiwa na Israel baada ya kulikamata katika vita vya mwaka 1967. Udhibiti huo wa Israel hautambuliwi chini ya sheria ya kimataifa.

Syria yasema Marekani imeipendelea Israel

Shirika la habari la Syria limenukuu chanzo kutoka wizara ya mambo ya kigeni na kusema Rais Donald Trump ameonesha upendeleo wa Marekani kwa Israel na kwamba hatua hiyo haiwezi kubadili ukweli, na eneo hilo litabaki kuwa la Syria. Kwa upande wake Iran imesema, kauli ya Trump haikubaliki na siyo halali huku Urusi ikieleza kwamba kubadili hali ya eneo la Golan ni kuvunja maazimio la umoja wa mataifa. Naye Rais wa Uturuki, Reccep Tayip Erdogan amelaani vikali pia tamko hilo la Trump na kusema, "Haiwezekani kutarajia kwamba Uturuki na Jumuiya ya nchi za kiislamu ikakaa kimya ama kunyamazia suala hili nyeti. Hatuwezi kuruhusu kuhalalishwa kuchukuliwa kwa eneo la Golan na kamwe hatutakubali''

Urusi na Iran pia zamkosoa Trump

Iran na Urusi inavyo vikosi nchini Syria ili kumuunga mkono Rais Bashar Al Assad katika vita vinavyoendelea nchini humo huku Iran ikipeleka vikosi vyake yenyewe na kupeleka wanamgambo wa kishia inaowasaidia kama vile Hezbollah. 

Golan Höhen israelische Soldaten Syrien
Wanajeshi wa Israel katika milima ya GolanPicha: Reuters/A. Cohen

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekuwa akiipa shinikizo Marekani kutambua madai ya nchi hiyo na kutoa dukuduku lake juu ya uwezekano wa eneo la Golan kutambuliwa kuwa la Israel na alizungumza juu ya hilo katika mkutano wake wa kwanza na Rais Donald Trump kwenye ikulu ya White house nchini Marekani mnamo mwezi Februari mwaka huu. 

Siku ya alhamisi Rais Donald Trump aliandika katika mtandao wa Twitter kwamba baada ya miaka 52, ni wakati muafaka kwa Marekani kutambua udhibiti wa Israel katika milima ya Golan, akiliita eneo hilo kuwa la kimkakati na kiusalama kwa Taifa la Israeli na uthabiti wa kanda nzima. Kauli hiyo ya Trump ilitafsiriwa kulenga kumsaidia Netanyahu katika kampeni ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi ujao.