1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria:Mashambulizi ya magharibi yakiuka sheria za kimataifa

Sekione Kitojo
14 Aprili 2018

Serikali ya Syria imeyaita mashambulizi ya mataifa ya magharibi kwenye mitambo yake ya kijeshi, kuwa ya kikatili na kijinga na kwamba yamekiuka sheria za kimataifa.

https://p.dw.com/p/2w2MR
Zypern Britischer Kampfjet vor Einsatz
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Matthews


Serikali ya Syria imeyaita mashambulizi ya mataifa ya magharibi kwenye mitambo yake ya kijeshi, kuwa ya kikatili na kijinga na kwamba yamekiuka sheria za kimataifa. Marekani, Ufaransa na Uingereza zimefanya mfululizo wa mashambulizi ya angani Jumamosi asubuhi katika maeneo ya karibu na mji mkuu wa Damascus na katikati mwa mji wa Homs.

Operesheni hiyo ya pamoja inakuja wiki moja baada ya shambulizi la kemikali linalodiawa kufanywa kwenye mji unaodhibitiwa na waasi nje kidogo ya Damascus na kuwaua watu 40. Mataifa ya magharibi yalimtuhumu rais Bashar al Assad kwa shambulizi hilo, lakini Syria na mshirika wake Urusi wamekana madai hayo na kuyatuhumu mataifa hayo kwa kutengeneza tukio hilo ili kuhalalisha hatua za kijeshi. 

Kundi la Hezbollah la nchini Lebanon, mshirika wa serikali ya Syria, limelaani mashambulizi hayo na kusema mataifa hayo hayatatimiza malengo yake. 

Miripuko  ilionekana  ikitoa mwanga  katika  anga la mjini  wa Damascus, mji  mkuu wa Syria, wakati  Trump akizungumza  kutokea  Ikulu  ya White House.

Televisheni  ya  Syria  imeripoti  kwamba  vifaa vya ulinzi wa anga  nchini Syria , ambao  ni  muhimu , vilijibu  shambulio  hilo. Baada  ya shambulio  kusita  na  hali  kutulia, magari  yakiwa  na  vipaza  sauti yaliingia  mitaani  katika  mji  mkuu  Damscus yakipiga  muziki  wa kauli  mbiu  za  kitaifa.

USA - Trump ordnet Militärschlag auf Syrien an
Rais Donald Trump akizungumza kutoka Ikulu ya White House Picha: Getty Images/AFP/M. Ngan

Trump alisema  Marekani  iko  tayari  kuendelea  na  mbinyo  dhidi ya  Assad  hadi  pale  atakapofikisha  mwisho  kile  rais  huyo alichosema  utaratibu  wake  wa  kihalifu wa  kuwauwa raia  wake kwa  silaha  za  sumu  zilizopigwa  marufuku  kimataifa. Haijafahamika  mara  moja  iwapo  Trump  alikuwa  na  maana kwamba  operesheni  hiyo  ya  kijeshi  ya  washirika  itaendelea zaidi  ya  mashambulio  hayo  ya  awali  ya  makombora.

"Shambulio  la uovu na la  kinyama  limesababisha  wakina mama  na baba , watoto wachanga  na  vijana , wakitapia  maisha  yao kwa kukosa  hewa. Haya  si  matendo  ya  kibinadamu , badala  yake  ni uhalifu  wa  zimwi,"  alisema  Trump.

Syrien Militärschlag Flugzeug
Ndege za mataifa washirika zikijitayarisha kushambulia SyriaPicha: Reuters/Twitter/French Military

Waziri  mkuu  wa  Uingereza  Theresa May  alisema  mjini  London kwamba  mataifa  ya  magharibi  yamejaribu "kila  kinachowezekana" kwa  njia  ya  kidiplomasia  kumzuwia Assad  dhidi  ya  kutumia silaha  za  sumu. "Lakini  juhudi  zetu kila  mara  zimezuiwa" na  Syria na Urusi, amesema.

Kubadili  utawala

"Kwa  hiyo  hakuna  nafasi  mbadala  ila  kutumia  nguvu  kuharibu na  kuizuwia  serikali  ya  Syria  kutumia  ya  silaha  za  sumu," May alisema.

"Hii  haihusiani  na  kuingilia  kati  katika  vita  vya  wenyewe  kwa wenyewe.  Haihusiani  na  kubadilisha  utawala."

Syrien - Militärschlag - Theresa May
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: picture alliance/AP Photo/UK Government

Rais  wa  Ufaransa  Emmanuel Macron  alisema  katika  taarifa kwamba  lengo  la  shambulio  hilo lilikuwa  hazina ya  silaha  za sumu iliyofichwa  na  serikali  ya  Syria."

Trump  hakutoa maelezo juu  ya  shambulio  hilo  la  pamoja  la Marekani, Uingereza  na  Ufaransa, lakini  ilikuwa  inatarajiwa kujumuisha  makombora  kadhaa  yaliyorushwa  kutoka  nje  ya  anga la  Syria. Amefafanua  lengo  kuu  kuwa  ni  kuonesha  upinzani mkubwa  dhidi  ya  matumizi  ya  silaha  za  sumu.

Serikali  ya  Syria  imekana  mara  kadhaa  kutumia  silaha zilizopigwa  marufuku.

Syrien - Militärschlag - Emmanuel Macron
Rais Emmanuel Macron katika mkutano uliohusu shambulizi la pamoja dhidi ya SyriaPicha: Reuters/Twitter/Emmanuel Macron

Stoltenberg  aunga  mkono shambulio

Uamuzi  wa  kushambulio , baada  ya  siku  kadhaa  za  majadiliano, ni  hatua  ya  pili  ya  Trump  kuamuru  shambulio  nchini  Syria.

Aliamuru kushambuliwa  kwa  kituo  cha  kijeshi  nchini  Syria  mwezi Aprili 2017  kwa  makombora  kadhaa  chapa  Tomahawk kwa kulipiza  kisasi  dhidi  ya  utawala  wa  Assad  kutumia   gesi  ya sarin   dhidi  ya  raia.

Katibu  mkuu  wa  jumuiya  ya  NATO  Jens Stoltenberg  ameelezea kuunga  kwake  mkono  mashambulizi  ya  anga  ya  mataifa  ya magharibi  nchini  Syria  leo Jumamosi baada  ya  shambulio lililolenga  utawala  wa  Bashar al-Assad  ikiwa  ni  jibu  kwa shambulio  linaloshukiwa  kufanywa  na  utawala  huo  la  silaha  za sumu. Naunga  mkono  shambulio  lililofanywa na Marekani, Uingereza  na  Ufaransa , hii  itapunguza uwezo  wa  utawala  wa Syria  kuwashambulia  zaidi  watu  wake  kwa  silaha  za  sumu," amesema  Stoltenberg.

Belgien Nato weist wegen Giftanschlags sieben russische Diplomaten aus
Jens Stoltenberg katibu mkuu wa NATOPicha: Getty Images/AFP/E. Dunand

Katika  wizara  ya  ulinzi  ya  Marekani , waziri  wa  ulinzi Jim Mattis alisema  shambulio  hilo  lilikuwa  kubwa  dhidi  ya  serikali  ya  Syria kuliko  ilivyokuwa  mwaka  2017 na lililenga  miundo mbinu  ya  silaha za  sumu  nchini  Syria. Alilieleza  shambulio  hilo  kuwa  ni "pigo moja," na  kuongeza, "Naamini  limefikisha  ujumbe  mzito."

Mwandishi: Sekione  Kitojo / ape

Mhariri: Isaac Gamba