1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yahimizwa kutoa nafasi kwa misaada ya kigeni

MjahidA25 Julai 2013

Wajumbe wawili wa Umoja wa Mataifa wako mjini Damascus kuihimiza serikali ya Syria kuwakubalia maafisa wake kuingia nchini humo kuchunguza matumizi ya silaha za kemikali, yanayodaiwa kutumika katika miezi 28 ya ghasia

https://p.dw.com/p/19E3W
Rais wa Syria Bashar al-Assad
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture alliance/dpa

Serikali ya Bashar Al Assad na waasi wanaopigana kuiondoa serikali hiyo madarakani wamekuwa wakinyosheana kidole cha lawama kwa matumizi ya silaha za kemikali katika ghasia za nchi hiyo zilizosababisha watu takriban 100,000 kuuwawa huku wengine wengi wakikimbia maakazi yao.

Kulingana na wanasayansi kutoka Sweden Ake Sellstrom na Angela Kane, wawakilishi wakuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya silaha wamewasili mjini Beirut kwa mazungumzo, ambayo yamekuwa yakishinikizwa na Umoja huo kufanyika tangu mwezi wa Aprili.

Wanajeshi wa Syria
Wanajeshi wa SyriaPicha: picture-alliance/dpa

Wawakilishi hao wanatarajiwa kukutana na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Syria Walid Muallem.

Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu ilionya jana kwamba maelfu ya raia wa Syria wana mahitaji makubwa ya msaada wa kibinaadamu ambao unazuiwa kuwafikia na maafisa wa serikali ya Assad.

Kamati hiyo iliyo na makao yake makuu mjini Geneva imesema mji unaohitaji msaada huo kwa haraka ni Homs, ambao umekumbwa na mapigano makali zaidi tangu kuanza kwa machafuko mwaka wa 2011.

John Kerry kukutana na kiongozi wa Upinzani

Hata hivyo ziara ya wawakilishi hao wa Umoja wa Mataifa imekuja wakati upande wa upinzani ukisema kwamba Saudi Arabia wameendeleza juhudi za kutoa silaha kwa waasi kwa matayarisho ya mashambulizi makubwa mjini Allepo na maeneo yanayoshikiliwa na serikali kaskazini mwa mji huo.

Ziara hii pia imekuja baada ya mkutano wa kiongozi wa upinzani Ahmad Jarba na rais wa Ufaransa Francois Hollande mjini Paris. Jarba aliiomba Ufaransa kuendelea kuunga mkono upinzani kisiasa, kidiplomasia, msaada wa kibinaadamu na wa kijeshi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry sasa atakutana na kiongozi huyo wa upinzani hii leo kandoni mwa mkutano wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa unaofanyika mjini New York Marekani.

Waziri wa nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry
Waziri wa nchi za Kigeni wa Marekani John KerryPicha: Reuters

Huu utakuwa mkutano wa kwanza kati Kerry na Jarba tangu Jarba alipochaguliwa mkuu wa upinzani nchini Syria Julai 6.

Kwa Upande wake Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za kigeni wa Marekani Jen Psaki amesema katika mazungumzo hayo Kerry atawasilisha ujumbe wa Marekani kwamba imejitolea kuendelea kusaidia kuupa nguvu upinzani nchini Syria.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman