Syria kukubaliana na mapendekezo ya Jumuiya ya Kiarabu | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.11.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Syria kukubaliana na mapendekezo ya Jumuiya ya Kiarabu

Mwakilishi wa Syria kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Youssef Ahmed, amewasili mjini Cairo akipeleka jibu la nchi yake kwa mpango uliopendekezwa na Jumuiya hiyo kumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea Syria.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad.

Rais wa Syria, Bashar al-Assad.

Hapo jana (01.11.2011) Shirika la Habari la Syria (SANA) lilitangaza kuwa makubaliano yamekwishafikiwa kati ya Syria na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, lakini Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo, Ahmed Bin Helli, amesema mapema leo kwamba walikuwa hawajapata jibu lolote kutoka kwa Syria.

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Cairo asubuhi ya leo, Ahmed amethibitisha kuwa ana majibu ya Syria kwa mpango uliopendekezwa na Jumuiya hiyo, katika juhudi za kuutanzua mzozo wa kisiasa ambao umekuwa ukiigubika Syria kwa muda wa miezi minane sasa.

''Nitaongoza ujumbe wa Syria kwenye mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Mataifa ya Kiarabu na nitawasilisha jibu la nchi yangu kwenye mkutano huu juu ya pendekezo la kumaliza mzozo unaoendelea kwetu.'' Amekaririwa Ahmed na Shirika la Habari la Ujerumani (DPA). Hata hivyo, mwanadiplomasia huyo alikataa kueleza undani wa jibu hilo.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa kwa uchache watu 3000, wengi wao wakiwa raia, wamekwishapoteza maisha yao katika machafuko ya miezi minane nchini Syria.

Waandamanaji wakiomba marufuku ya kuruka ndege nchini Syria.

Waandamanaji wakiomba marufuku ya kuruka ndege nchini Syria.

Mwezi uliopita, Marekani, Uingereza na Ufaransa zilipendekeza kwenye Baraza la Usalama wa Umoja wa Mataifa kwamba Syria iwekewe vikwazo zaidi ya vile vilivyowekwa hadi sasa, lakini pendekezo hilo lilikwamishwa na kura za turufu za Russia na China.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Lavlow, akiongelea kuhusu msimamo wa nchi yake juu ya Syria, alisema baada ya maelfu ya vifo vya raia nchini Libya, Russia haipendi kuona hayo yakitokea kokote kwingineko.

''Sisi hatuungi mkono serikali, tunaunga mkono sheria ya kimataifa. Tukitilia maanani maelfu ya vifo yaliyotokea nchini Libya chini ya kaulimbiu ya kuwalinda raia, na tukikumbuka wito uliotolewa baadaye na katibu mkuu wa NATO kuwa hayo yaliyotokea Libya ni mfano wa kuigwa, tusingependa kuona hali hiyo ikirudiwa mahali pengine.'' Alisema Lavrov.

Pendekezo la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kwa Syria linaitaka serikali ya Rais Bashar al-Assad kuachia wafungwa wote wa kisiasa, kuondoa vikosi vya usalama mitaani, kuwaruhusu waangalizi wa Jumuiya hiyo nchini Syria na kuanza mazungumzo na upinzani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPA
Mhariri: Othman Miraji

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com