1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Suu Kyi ajibu tuhuma za mauaji ya halaiki

11 Desemba 2019

Waziri Mkuu wa Myanmar Aung San Suu Kyi anatoa ushahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague Uholanzi. Amekanusha madai kuwa Myanmar ilifanya mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa Rohingya

https://p.dw.com/p/3Ub8O
Niederlande Den Haag Aung San Suu Kyi vor dem Internationalen Gerichtshof
Picha: picture-alliance/AP Photo/P. Dejong

Mahakama hiyo ya juu kabisa ya Umoja wa Mataifa ilianza jana vikao vya kusikiliza kesi kuhusu madai ya mauaji ya halaiki dhidi ya watu wa jamii ya wachache ya Rohingya nchini Myanmar.

Mshindi huyo wa tuzo ya amani ya Nobel Aung Sang Suu Kyi ameiambia mahakama hiyo ya juu ya Umoja wa Mataifa kuwa madai kwamba Myanmar ilifanya mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa Rohingya ni "ya kupotosha na yasiyo kamilifu."

Kesi hii ilifikishwa mbele ya mahakama hiyo na Gambia ikiitaka korti hiyo ya ulimwengu ichukue hatua zote zilizoko ndani ya uwezo wake kuzuia vitendo ambavyo vinachangia uhalifu wa mauaji ya halaiki. Suu Kyi amesema Gambia imewasilisha mbele ya mahakama picha isiyokuwa ya kweli na kuiambia mahakama kuwa hakuna ushahidi wa „nia ya kufanya mauaji ya halaiki, katika kampeni ya jeshi la nchi yake dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Akizungumza jana mahakamani, Waziri wa sheria wa Gambia, Abubacar Tambadou alisema lengo la kesi hiyo ni kuitaka Myanmar kuacha mauaji ya kikatili. Kukomesha hivi vitendo vya kinyama ambavyo vimeushangaza ulimwengu.

Niederlande Justiz l Unterstützung für Min Aung Hlaing vor dem Internationalen Gerichtshof in Den Haag
Watu wa Myanmar wakimuunga mkono kiongozi waoPicha: DW/A. Islam

Serikali ya nchi hiyo iliyo kusini mashariki mwa Asia inadaiwa kupanga mauaji ya halaiki ya Waislamu walio wachache nchini humo Warohingya. Mwaka 2017 maelfu ya Warohingya walikimbilia nchi jirani ya Bangladesh baada ya mashambulizi ya polisi na wanajeshi yaliyoitikisa nchi hiyo.

Suu Kyi, ambaye ni kiongozi wa ngazi ya juu kabisa wa kisiasa nchini Myanmar, aliwashangaza wakosoaji wake na kuwafurahisha waungaji mkono wake nyumbani aliposafiri kwenda The Hague kuongoza ujumbe wa serikali yake. Ofisi yake ilisema alikwenda kuyalinda maslahi ya kitaifa.

Anakosolewa pakubwa kutokana na kuchelewa kwake kuzungumzia udhalimu huo. Mahakama ya Juu ya Umoja wa Mataifa ilifungua kesi dhidi ya serikali ya Myanmar baada ya serikali ya Gambia kuweka shinikizo. Vikao hivyo vya kusikilizwa kesi ya Myanmar vitakamilika kesho Alhamisi.