Sudan zazidi kukamiana | Matukio ya Afrika | DW | 17.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Sudan zazidi kukamiana

Sudan imezidisha mashambulizi katika mji wenye utajiri mkubwa wa mafuta wa Heglig ulioko mpakani mwake na Sudan Kusini katika mapambano yanayotishia kuzipeleka nchi hizo vitani.

Marais Salver Kiir na Omar el Bashir

Marais Salver Kiir na Omar el Bashir

Katika mashambulizi yaliyofanyika siku ya jana, taarifa zinasema makombora ya ndege za Sudan yalizishambulia ofisi za Umoja wa Mataifa ingawa hakukuwa na majeruhi wowote waliyoripitiwa.

Sudan Kusini yanena
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini Kanali Philip Aguer alisema ndege mbili za Sudan ziliangusha mabomu kadhaa katika mji huo wa Heglig, wakati makombora ya masafa marefu yakilenga shabaha za majeshi ya Sudan Kusini katika mji huo unaogombaniwa na mataifa hayo mawili. Kanali Aguer alisema pia majeshi ya Sudan yaliua raia watano katika mashambulizi ya angani siku ya jumapili.

Gari lililoshambuliwa katika mapigano kati ya Sudan mbili

Gari lililoshambuliwa katika mapigano kati ya Sudan mbili

Alisema makombora hayo pia yaliushambulia mji wa Bentiu katika jimbo la Unity na kwamba mzozo huo sasa umeanza kusambaa katika majimbo mengi ya kusini mpakani mwa Sudan, ikiwa ni pamoja na magharibi mwa jimo la Bahrel el Ghazal, lakini akaongeza kuwa majeshi ya pande mbili yalikuwa hayajapambana moja kwa moja wiki hii.

Afisa mmoja wa Sudan naye alisema siku ya jumatau kuwa majeshe yake yamechukuwa udhibiti wa eneo la Mugum ambalo ni ngome kuu ya majeshi ya Sudan kusini katika jimbo la Bluu Nile karibu na mpaka wa Sudan Kusini.

Umoja wa Mataifa walaani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alieleza kustushwa kwake siku ya jumatatu na kuongezeka kwa wanamgambo katika jimbo la Abyei, ambalo ndiyo chanzo cha mzozo baina ya Sudan mbili. Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Eduardo del Buey alisema Ban amezitaka pande hizo mbili kumaliza mapigano haraka na kuheshimu sheria za kimatifa na pia kulinda raia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa ambaye ndiye Rais wa Baraza la Usalama kwa sasa, Suzani Rice alilaani mashambulizi ya jumatatu na kusema kuwa Umoja wa Mataifa unaalani mashambulizi dhidi ya ofisi zake.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini iliripoti matukio matatu ya mashambulizi ya angani katika jimbo la Unity, mawili katika mji wa Bentiu na lingine katika eneo la Mayom ambapo makao makuu ya walinda amani wa Umoja wa mataifa yalipigwa na bomu.

Sudan yaapa kuitia adabu Kusini
Msemaji wa Serikali ya Sudan alisema hakutakuwa na mazungumzo na serikali ya Sudan kusini hadi pale serikali yake itakaporejesha mji wa Heglig. Alisema wananchi wa Sudan wana hasira na kwamba huu si wakati wa diplomasia, bali ni wakati wa kupambana na kuionyesha Sudan Kusini kuwa inapaswa kuwajibika.

Baadhi ya wachambuzi wanasema mzozo huu baina ya Sudan mbili unaweza kufikia hatua ya vita kamili kabla nchi mbili hazijakaa na kufanya mazungumzo. Lakini Angelo Izama, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka Mjini Kampala, aliuelezea mzozo huu kuwa ni wa kipumbavu kwa kuzingatia kuwa nchi hizi bado zina masuala muhimu ya kusuluhisha.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\RTRE
Mhariri: Saum Yusuf.