1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yashambulia kambi ya Umoja wa Mataifa

16 Aprili 2012

Mzozo baina ya Sudan mbili unaendelea kupanuka ambapo sasa jeshi la Sudan ya Kusini linaishutumu serikali ya Sudan kwa kujaribu kuanzisha mashambulizi mengine katika eneo la kaskazini mashariki ya nchi yake.

https://p.dw.com/p/14eXG
Wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Sudan.
Wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Sudan.Picha: Reuters

Waziri wa habari katika jimbo la Unity amesema ndege za kijeshi za Sudan zimeishambulia kambi iliyoko kwenye eneo la Mayom katika jimbo hilo lenye mafuta la Sudan kusini huku, mashambulizi mengine yakisababisha vifo vya watu tisa.

Jana serikali ya Sudan iliionya jirani yake, Sudan Kusini, dhidi ya kuviharibu vinu vyake vya mafuta kwenye eneo la Hegling ambalo kwa sasa liko mikononi mwa wanajeshi wa Sudan Kusini. Onyo hilo limetolewa baada ya upande wa Sudan Kusini kuituhumu Khartoum kwa kuwaamrisha wanajeshi wake kulishambulia eneo hilo.

Akitoa onyo hilo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Sudan, Al Obeid Meruh, alisema ikiwa jeshi la kusini litaharibu kinu chochote cha mafuta itamaanisha kwamba iko tayari kupanua mgogoro huo katika kiwango kipya.

Hata hivyo jeshi la Kusini nalo linasema ndege za kivita za wanajeshi wa Sudan zimekuwa zikishambulia bila kujali katika eneo la Heglig ingawa halijafanikiwa kuwaondoa wanajeshi wa Kusini katika eneo hilo lenye utajiri wa mafuta linalozozaniwa na pande zote mbili.

Sudan ya Kusini kuondoka baada ya Sudan kujiondoa

Mwishoni mwa wiki, kiongozi wa ujumbe wa mazungumzo ya upatanishi wa Sudan ya Kusini, Pagan Amum, alisema ni kwa Sudan kuondoka tu kwenye maeneo mengine, ndipo majeshi ya nchi yake yataondoka Heglig

Mgogoro wa Sudan unaelekea kubaya.
Mgogoro wa Sudan unaelekea kubaya.Picha: picture alliance/landov

"Tuko tayari kujiondoa Heglig kama eneo linalogombaniwa, tukiamini kwa hakika kuwa ni sehemu ya Sudan ya Kusini. Lakini tutakubali kuondoka ikiwa pande zote husika zitaondoka kwenye maeneo yote yanayogombaniwa." Alisema Amum.

Waziri wa habari wa Sudan, Abdullah Ali Massar, amekanusha juu ya kushambuliwa kwa eneo la Heglig na wanajeshi wa nchi yake. Siku ya Jumamosi wanajeshi wa Sudan Kaskazini walidai wako kilomita chache kutoka mji wa Heglig, baada ya kuanzisha mashambulizi ya kulipiza kisasi. Hata hivyo, msemaji wa jeshi hilo hakujibu simu yoyote aliyopigiwa hadi kufikia jana.

Serikali ya Sudan imewapiga marufuku waandishi wa habari pamoja na mashirika ya misaada na wanadiplomasia kuingia jimbo la Kordofan Kusini ambalo mji wa Heglig ni sehemu yake na kuifanya hali ya mzozo huo kuwa ngumu kuthibitishwa.

Nchi zenye nguvu duniani zimeanza kuingiwa na wasiwasi kufuatia mapigano ya majirani hao wawili na hivyo kutoa mwito kwa pande zote mbili kujizuwia na mapigano.

Ni mara ya kwanza kushuhudiwa mapambano makali baina ya Sudan hizo mbili, tangu mwezi Julai baada ya upande wa Kusini kujitenga kufuatia kura ya maoni iliyofanyika kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyomaliza vita vya miaka 22 vya wenyewe kwa wenyewe.

Mwandishi: Saumu Yusuf/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef