Sudan yasema yakaribia kukamilisha mkataba na Marekani | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Sudan yasema yakaribia kukamilisha mkataba na Marekani

Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Asma Abdalla asema nchi hiyo inakaribia kukamilisha mkataba na Marekani wa fidia kwa waathiriwa wa shambulizi la mabomu katika balozi za Kenya na Tanzania ambapo watu 24 walifariki

Abdalla ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kwasasa kuna ujumbe mjini Washington unaojadiliana na mawakili wa waathiriwa hao katika wizara ya mambo ya kigeni. Mashambulizi hayo ya mabomu yalifanyika mnamo Agosti 1998 wakati mlipuko mkubwa ulipotokea katika ubalozi wa Marekani jijini Nairobi na kufuatiwa muda mfupi na mlipuko mwingine jijini Dar es Salaam.

Mashambulizi hayo yaliodaiwa kufanywa na kundi la wanamgambo la Al-Qaeda, yalisababisha vifo vya watu 224 na kujeruhi wengine kiasi ya 5000 karibu wote wakiwa waafrika. Marekani imeishtumu Sudan kwa kuwasaidia wanamgambo wanaohusishwa na mashambulizi hayo yaliofanywa na  kundi la itikadi kali na kutaka fidia kwa familia za wahanga.

Uongozi wa Sudan baada ya kuondolewa kwa Omar al-bashir

Tangu kuondolewa mamlakani kwa rais Omar al- Bashir baada ya wimbi la maandamano makubwa dhidi ya uongozi wake, Sudan imekuwa ikitawaliwa na serikali ya mpito. Chini ya uongozi wa miaka 30 ya Bashir, taifa hilo lilichukuwa mkondo wa msimamo mkali wa kiislamu, na kuwa mwenyeji wa mwanzilishi wa kundi hilo la Al- Qaeda Osama bin Laden kati ya mwaka 1992-1996.

Hatua hiyo ilivuruga uhusiano kati ya taifa hilo na Marekani ambayo iliiorodhesha Sudan kama taifa linalofadhili shughuli za kigaidi. Serikali ya sasa imetafuta kuimarisha nafasi ya kimataifa ya taifa hilo na kujenga upya uhusiano wake na Marekani.Mnamo mwezi Februari, ilibidi Sudan kulipa fidia kwa familia za waathiriwa wa shambulizi dhidi ya meli ya Marekani ya USS Cole mwaka  2000  katika bandari ya Aden nchini Yemen ambalo kundi la Al-Qaeda pia lilidai kuhusika.

Sudan imekanusha kuhusika katika mashambulizi hayo lakini imekubali kulipa fidia hii ikiwa ni moja ya matakwa ya Marekani ya kuiondoa katika orodha hiyo ya ugaidi. Abdalla amesema kuwa baada ya makubaliano hayo ya mashambulizi katika balozi hizo, Sudan itakuwa imekamilisha matakwa yote ya kuondolewa katika orodha ya mataifa yanayofadhili ugaidi.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com