1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan ya Kusini yaituhumu Sudan 'kuwatisha' wawekezaji

3 Aprili 2012

Licha ya Sudan na Sudan ya Kusini kufanya mazungumzo ya kutatua mzozo baina yao, hali ya kutokuaminiana inaongezeka huku Sudan ya Kusini ikisema Sudan inavishambulia visima vyake vya mafuta ili kuwatisha wawekezaji.

https://p.dw.com/p/14Wus
Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini.
Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini.Picha: picture alliance / ZUMA Press

Kauli hiyo ilitolewa na msemaji wa serikali ya Sudan ya Kusini, Barnaba Marial Benjamin, hapo jana jijini Nairobi katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Marial amesema kwamba licha ya makubaliano ya Februari 10 kati ya Sudan hizo mbili, uliosainiwa chini ya usimamizi wa Umoja wa Afrika, mjini Addis Ababa, Ethiopia, bado Sudan inayashambulia maeneo yanayobishaniwa baina yao, ambayo yana utajiri wa mafuta.

Marial, ambaye pia ni waziri wa habari wa serikali ya Sudan ya Kusini, amedai kwamba sababu ya Sudan kuyashambulia maeneo yanayozalisha mafuta ndani ya nchi yake, ni serikali ya Sudan ya Kusini kusitisha uzalishaji wa mafuta hapo mwezi Januari. Sudan ya Kusini iliyojitangazia uhuru wake katikati ya mwaka jana, iliamua kufunga uzalishaji wa mafuta ikidai kuwa Sudan ilikuwa inaiba mafuta yake.

Sudan yakana

Lakini Sudan imeziita tuhuma hizo kuwa ni za uzushi na zisizo na mashiko. Taarifa iliyotolewa na ujumbe wa Sudan kwenye mazungumzo yanayoendelea mjini Addis Ababa kati ya nchi hizo, imesema badala yake ni Sudan ya Kusini ndiyo ambayo imelishambulia eneo la Sudan.

Rais Omar Bashir wa Sudan.
Rais Omar Bashir wa Sudan.Picha: picture alliance / Photoshot

Katika siku za karibuni, jumuiya ya kimataifa imekuwa ikitiwa na shaka na uwezekano wa kuzuka tena vita kati ya pande hizo mbili kufuatia mapigano ya mpakani ya mwezi uliopita.

Rais Barack Obama wa Marekani anaripotiwa kumpigia simu Rais Salva Kiir wa Sudan ya Kusini, na kumuomba ayazuie majeshi yake kujiingiza kwenye vita na pia kutokuyaunga mkono mapigano ya mpakani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Marekani, Rais Obama alizungumza kwa njia ya simu na Rais Kiir na kumwambia kuwa "ni muhimu sana kwa mataifa mawili ya Sudan na Sudan ya Kusini kufikia makubaliano kuhusiana na rasilimali ya mafuta."

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amezitaka serikali zote mbili kuacha mara moja uadui baina yao na kutekeleza makubaliano yaliyokwishafikiwa baina yao juu ya masuala ya usalama, ulinzi wa mipaka na eneo la mpakani linalowaniwa la jimbo la Abyei.

Rais Barack Obama wa Marekani.
Rais Barack Obama wa Marekani.Picha: Reuters

Msemaji wa Ban Ki-moon, Martin Nesirky, amesema Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amemtaka Rais Omar Bashir wa Sudan kukutana na mwenzake Salva Kiir wa Sudan Kusini, haraka iwezekanavyo.

Mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika leo mjini Juba, Sudan ya Kusini, kati ya marais hao wawili, ulisitishwa na serikali ya Sudan, kwa sababu ya kuendelea kwa mapigano ya mpakani.

Hata hivyo, Waziri wa Habari wa Sudan ya Kusini, Benjamin Marial, amesema kwamba licha ya mashambulizi yanayofanywa na Sudan dhidi ya nchi yake, bado Sudan ya Kusini inataka Bashir na Kiir wakutane.

Mwandishi: Mohammed Khelef /AP/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman