Sudan walaumiana vifo vya waandamanaji | Matukio ya Afrika | DW | 01.07.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Sudan walaumiana vifo vya waandamanaji

Waandamanaji nchini Sudan wamelitupia lawama baraza la kijeshi linalotawala nchini humo baada ya kupatikana kwa miili mitatu iliyokuwa na damu, siku moja baada ya kufanyika maandamano mengine mapya baada ya yale ya Juni.

Vikosi vya usalama viliyazima maandamano hayo kwa hatua kali dhidi ya waandamanaji.

Mapema leo maiti tatu zilizokuwa na damu zilikutwa katika mitaa ya Amdurman mjini Khartoum ambako maandamano hayo yalifanyika. Kundi la watu liliizunguka miili hiyo na muda mfupi baadae kutawanywa na polisi wa kutuliza ghasia kwa gesi ya kutoa machozi. Miili hiyo haijatambuliwa.

Vyombo vya habari vya serikali vimeripoti watu saba wameuawa, wakati maelfu wakiandamana wakishinikiza iundwe serikali ya kiraia huku kamati ya madaktari inayojishikamanisha na waandamanaji hao ikisema ni waandamanaji watano waliouawa.

Maandamano kwenye taifa hilo la kaskazinimashariki mwa Afrika yamelenga kushinikiza kuondoka kwa majenerali waliohodhi madaraka kufuatia kuondolewa kwa aliyekuwa rais Omar al-Bashir mwezi Aprili.

Sudan Bashir (picture-alliance/AP Photo/M. Hjaj)

Rais Omar al-Bashir akisindikizwa kurudi mahabusu kufuatia madai ya rushwa

Maandamano hayo yaliyofanyika jana Jumapili yameonekana kama mtihani kwa waratibu wa maandamano baada ya kambi ya waandamanaji kuvamiwa mnamo Juni 3 katika mji mkuu Khartoum na kusababisha vifo vingi na kufungwa kwa huduma za intaneti hatua iliyopunguza kasi ya uhamasishaji.

Mwandishi wa habari wa shirika la AFP na mashuhuda wamesema hatua hiyo haikuweza kuzuia wimbi kubwa la waandamanaji wanawake kwa wanaume waliojitokeza katika mitaa pacha ya Omdurman katika mji mkuu wa Khartoum pamoja na miji na majiji mingine wakiimba nyimbo zinazodai utawala wa kiraia.

Sudan Khartum | Protest gegen Militärregierung | Einsatz von Tränengas (Reuters/M.N. Abdallah)

Vikosi vya usalama vikikabiliana na waandamanaji katika mitaa ya Khartoum

Vikosi vya usalama vimeimarisha ulinzi kwa kuongeza idadi kubwa ya wanajeshi katika maeneo muhimu ya Khartoum, wakifyatua gesi ya kutoa machozi kwenye maeneo kadhaa na dhidi ya waandamanaji, wanaojaribu kuyafikia makaazi ya rais.

Shirika rasmi la habari la SUNA limemnukuu afisa wa wizara ya afya akisema pamoja na watu hao saba waliouawa, wengine 181 walijeruhiwa, miongoni mwao 27 waliojeruhiwa kwa risasi za moto, na wanajeshi 10 pia wamejeruhiwa.

Kiongozi maarufu wa waandamanaji Mohamed Naji al-Assam ameonekana akilitupia lawama baraza la kijeshi kuwa ndio chanzo cha vifo hivyo kwenye ukanda wa video aliouchapisha kwenye ukurasa wa Facebook huku majenerali hao wakiwalaumu waandamanaji kwa machafuko hayo ya jana.

Hali ya wasiwasi imeendelea kuwa juu kati ya viongozi wa waandamanaji na majenerali wa kijeshi tangu hatua kali za kijeshi dhidi ya waandamanaji za Juni 3. Wakati kamati ya madaktari wakisema idadi ya vifo imefikia 133, wizara ya afya inasisitiza ni 68 tu wamekufa.

Ethiopia na Umoja wa Afrika wamekuwa wakisuluhisha pande hizo mbili lakini bado hakujapatikana suluhu.

 

DW inapendekeza