1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan: Waandamanaji wawili wauawa kwa kupigwa risasi

Sylvia Mwehozi
15 Februari 2022

Waandamanaji wawili wameuawa kwa kupigwa risasi wakati vikosi vya usalama vilipokabiliana na umati wa watu, waliokuwa wakiandamana nchini Sudan wakipinga utawala wa kijeshi na kushinikiza kuachiliwa kwa wanaharakati.  

https://p.dw.com/p/471D4
Protest für die Zivilverwaltung im Sudan
Picha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Maelfu ya raia walimiminika tena katika mitaa ya mji mkuu wa Khartoum na mji pacha wa Omdurman na pia katika miji mingine, wakiendelea kupinga mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Oktoba. Waandamanaji wanataka mamlaka ziwaachie huru wanaharakati waliokamatwa huku wengine walionekana wakiwa wamebeba picha za wenzao waliouawa. Soma Raia mwingine auawa katika maandamano ya Khartoum

Tume huru ya madaktari wa Sudan imesema mwandamanaji mmoja aliuawa mjini Khartoum baada ya kupigwa risasi "shingoni na kifuani" na mwingine aliuawa baadaye mjini Omdurman naye akipigwa risasi katika "bega la kushoto iliyopenya hadi kifuani".

Polisi nayo imesema maafisa wake 102 "wamejeruhiwa vibaya" na mmoja ana "jeraha la risasi mguuni". Polisi hao walitumia mabomu ya kutoa machozi kutawanya umati wa watu waliokaribia jengo la bunge ambalo halitumiki mjini Omdurman.  Pia wanadai kuwa waandamanaji "walivunja sehemu ya mbele" ya jengo la bunge, kuchoma moto kituo cha mafuta kilicho karibu, na kuharibu magari kadhaa na msikiti huko Omdurman.

Protest für die Zivilverwaltung im Sudan
Maandamano ya Jumatatu mjini KhartoumPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Uharibifu mwingine pia umeripotiwa katika sehemu kadhaa za wizara ya vijana na michezo katika jiji hilo, na baadhi ya vitu vya walinzi viliporwa, ilisema taarifa hiyo ikiongeza kuwa polisi "walitumia nguvu kihalali" katika kuwakabili waandamanaji. Jeshi la Sudan limekuwa likikanusha mara kwa mara kuwafyatulia risasi waandamanaji, lakini shirika la Human Rights Watch limewanukuu mashahidi kadhaa wakieleza jinsi vikosi hivyo vinavyotumia risasi za moto na kurusha mabomu ya machozi dhidi yao. Idadi ya watu waliouawa tangu kuanza maandamano hayo imefikia 80.

Mamlaka pia zimewakamata wanaharakati kadhaa wanaotuhumiwa kuwa wanachama wa kamati za upinzani ambazo ndio zimekuwa zikiandaa maandamano. Kulingana na chama cha wanataaluma wa Sudan SPA, "idadi ya watu waliokamatwa kiholela na bila ya mashitaka ya jinai inazidi watu 100".

Katika gereza la Soba lililopo mjini Khartoum, watuhumiwa wameanzisha mgomo wa kula kupinga mazingira ya jela, kulingana na taarifa ya tume ya madaktari. Wakati huohuo kiongozi wa kijeshi wa Sudan Abdel Fattah al-Burhan, alikutana siku ya Jumatatu na balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini Sudan na kumkabidhi mwaliko kutoka kwa rais wa nchi hiyo Sheikh Khalifa bin Zayed Al-Nahyan. Umoja wa Falme za Kiarabu sambamba na Marekani na Uingereza zimehimiza juu ya kurejeshwa kwa utawala wa mpito wa kiraia nchini Sudan.