1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan kwazidi kutokota

Lilian Mtono
2 Julai 2019

Umoja wa Falme za Kiarabu umezitolea mwito pande zinazozozana nchini Sudan kuendelea na mazungumzo, na kujizuia na machafuko baada ya viongozi wa waandamanaji kuitisha kampeni ya siku moja ya uasi wa kiraia. 

https://p.dw.com/p/3LRpU
Sudan Demonstrationen in Omduran
Picha: Getty Images/AFP/Y. Chiba

Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu Anwar Gargash ameandika kwenye ukurasa wa twitter akisema ni muhimu kwa Sudan kuendeleza mazungumzo yatakayopelekea kupatikana kwa makubaliano ya mpito, lakini pia akiitaka kujiepusha na machafuko. 

Amesema, mabadiliko yoyote yatapaswa kuhakikisha kunaanzishwa mfumo thabiti wa kikatiba.

Viongozi wa waandamanaji nchini humo jana Jumatatu waliitisha kampeni hiyo ya uasi wa kiraia kwa nchi nzima ifikapo Julai 14, ikiwa ni siku moja baada ya kuandaa maandamano makubwa kabisa dhidi ya baraza tawala la kijeshi lililochukua mamlaka kufuatia kuondolewa mamlakani rais Omar al-Bashir mwezi Aprili.

Kulingana na viongozi wa waandamanaji, hatua zaidi za kuongeza shinikizo dhidi ya baraza hilo la kijeshi kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia, zinatarajiwa kuchochewa na maandamano makubwa zaidi ya Julai 13.

Sudan Khartum Massenproteste der Opposition
Waandamanaji wanaendelea kushinikiza kupatikana kwa utawala wa kiraiaPicha: AFP/A. Shazly

Viongozi hao wameitisha uasi wa kiraia ifikapo Julai 14, katika tangazo walilolitoa jana Jumatatu, siku moja baada ya kuandaa maandamano makubwa ya kulipinga baraza hilo la kijeshi, lililoitumbukiza nchi hiyo kwenye mzozo mkubwa wa kisiasa.

Kiongozi wa muungano wa uhuru na mabadiliko, Shareef Othman alinukuliwa akisema "Jumamosi ya tarehe 13 kutakuwa na maandamano ya Melloni na maandamano haya yatakuwa ni kwa ajili ya mauaji ya kikatili ya Arbainia na kukabidhiwa mamlaka ya kiraia katika maeneo ya Sudan, katika mji mkuu na vijiji vya Sudan Jumapili ya tarehe 14, itakuwa siku ya uasi wa kiraia na mgomo mkubwa wa kisiasa katika sekta zote za kitaaluma katika mji mkuu na maeneo mengine pamoja na maandamano nje ya Sudan."

Marekani yaingilia kati mgogoro huo

Mwito wa kampeni hiyo unakuja katika wakati ambapo pande hizo mbili zinazozozana zikilaumiana kwa machafuko wakati wa maandamano makubwa yaliyofanyika siku ya Jumapili na kusababisha vifo vya watu 10 na mamia wengine kujeruhiwa.

Makumi kwa maelfu waliandamana juzi Jumapili katika mitaa ya mji mkuu Khartoum na maeneo mengine, yakiwa ni maandamano makubwa zaidi kufanyika tangu vikosi vya usalama vilipowatawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika mbele ya jengo la wizara ya ulinzi, mwezi uliopita. 

Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, Stephane Dujarric amesema katibu mkuu huyo ameitolea mwito kwa mara nyingine Sudan kwa kuzitaka pande zote mbili kurejea kwenye mazungumzo ya kisiasa, ili kuundwa kwa serikali ya mpito haraka iwezekanavyo, lakini pia ametaka kuchukuliwa hatua kwa wahusika wa mauaji hayo ya juzi.

Marekani kwa upande wake imelaani matumizo ya risasi za moto dhidi ya waandamanaji, na kusema utawala wa kijeshi unapaswa kuwajibika kwa mauaji ya raia.