1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan Kusini yaunda kamandi ya pamoja ya vikosi vya jeshi

Babu Abdalla13 Aprili 2022

Serikali ya Sudan Kusini imetangaza jana Jumanne kuunda kamandi ya pamoja ya vikosi vya jeshi, ikiwa sehemu muhimu ya utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018.

https://p.dw.com/p/49suX
Zentralafrikanische Republik 2019 | Kämpfer der UPC
Picha: Florent Vergnes/AFP/Getty Images

Upepo wa matumaini unavuma nchini Sudan Kusini kufuatia tangazo la Jumanne la kuunda kamandi ya pamoja ya vikosi vya jeshi.

Jana Jumanne 12.04.2022, shirika la utangazaji la taifa la SSBC lilitangaza mfululizo wa amri za Rais Salva Kiir za kufanya mabadiliko katika vikosi vya jeshi, idara ya polisi na vikosi vyengine vya usalama.

Shirika hilo la habari limesema maagizo hayo mapya yataanza kutekelezwa mara moja.

Chini ya masharti hayo ya makubaliano yaliyotiwa saini Aprili 3, uundwaji wa kamandi ya pamoja ya jeshi unapaswa kukamilika ndani ya miezi miwili.

Sudan Kusini imeshuhudia vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mitano

Referendum Südsudan
Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir akionyesha kidole chenye wino baada ya kupiga kuraPicha: AP

Taifa hilo jipya zaidi duniani limekabiliwa na vita vya miaka mitano vya wenyewe kwa wenyewe kati ya wanajeshi watiifu kwa Rais Salva Kiir na wale wanaomtii mpinzani wake, makamu wa Rais Riek Machar.

Vita hivyo vimegharimu zaidi ya maisha ya watu 400,000 kabla ya viongozi hao wawili kutia saini mkataba wa maelewano mnamo mwaka 2018.

Licha ya makubaliano hayo, kuzuka kwa ghasia za mara kwa mara kunatishia kuirudisha nchi hiyo katika mzozo mwengine wakati pande mbili zinazohasimiana zikijipata kwenye mkwamo baada ya kutofautiana juu ya masuala kadhaa ikiwemo la uundaji wa kamandi ya pamoja ya jeshi- kipengele muhimu cha mkataba wa amani wa mwaka 2018.

Soma pia: Marekani : Sudan Kusini yashindwa kutekeleza amani

Mapema mwezi huu, Machar na Kiir walitia muhuri makubaliano juu ya kugawanya nafasi za juu kwenye kamandi hiyo mpya ya pamoja ya jeshi, wakikubaliana kugawanya asilimia 60-40 ya nafasi hizo huku upande wa Kiir ukichukua nafasi ya uongozi katika jeshi, polisi na vikosi vya usalama wa kitaifa.

Kulizuka mapigano mapya Ijumaa katika jimbo la Unity State

Licha ya makubaliano hayo, ghasia zinaendelea kushuhudiwa nchini humo baada ya kutokea kwa makabiliano mapya mnamo siku ya Ijumaa kati ya wanajeshi watiifu kwa Kiir na Machar.

Makabiliano hayo yamesababisha maelfu ya watu kuyakimbia maakazi yao katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Unity State.

Tangu kupata uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011, taifa hilo changa limetumbukia katika migogoro ya kila aina kuanzia mafuriko, baa la njaa, ghasia za kikabila na ukosefu wa utulivu wa kisiasa.

Soma pia: Sudan: Waandamanaji wawili wauawa kwa kupigwa risasi

Mwezi uliopita, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura ya kuongeza muda wa kuhudumu kwa ujumbe wake wa kulinda amani nchini humo kwa mwaka mmoja zaidi.

Umoja wa Mataifa mara kwa mara umeukosoa uongozi wa Sudan Kusini kwa kuchochea ghasia nchini humo na, umeishtumu serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu hatua ambayo huenda ikatafsiriwa kuwa uhalifu wa kivita kutokana na mashambulizi mabaya yaliyotokea kusini magharibi mwa nchi hiyo mwaka uliopita.